WAOMBA SERIKALI KUONDOA KODI VIFAA TIBA

Na Robert Kalokola,Geita

Baadhi ya wawekezaji katika sekta ya afya hapa nchini wameomba serikali kupunguza au kuondoq kodi katika vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi ili viweze kuwa na bei ambayo wanunuzi wengi watamudu kununua na kusaidia kutoa matibabu yenye viwango vya hali ya juu kwa wagonjwa.

Maombi hayo yametolewa na Afisa kutoka Kampuni inayouza na inayosambaza madawa ya binadamu pamoja na vifaa tiba hapa nchini ya Kas Medics, Patrick Ntakisigae na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Charles Kulwa Kata ya Runzewe wilayani Bukombe Mkoa wa Geita.

Wawekezaji hao wametoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Hospitali ya Charles Kulwa kwa kushirikiana na Kas Medics ili kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora wa Hospitali hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Said Nkumba akimkabidhi cheti na zawadi Mfanyakazi bora wa Hospitali ya kumbukumbu ya Charles Kulwa (Picha na Robert Kalokola).
 
Patrick Ntakisigae amesema kuwa, vifaa tiba vingi vina bei kubwa kwa sababu vinafanya kazi za kibingwa na vinatengenezwa kwa teknolijia ya kisasa hivyo ni vizuri serikali kuona njia nzuri ya kupunguza kodi ili bei iweze kupungua.

Amesema kuwa, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa uliofanywa na Serikali kwenye Hospitali zake na Hospitali za Sekta binafsi umesaidia wagonjwa wengi kutibiwa hapa nchini na kuokoa gharama kubwa za kusafiri kufuata matibabu hayo nje ya nchi.

Mtendaji Mkuu wa Kanda wa Kas Medics, Masilamani Guru alisema kuwa kampuni hiyo inatoa huduma za kuuza na kusambaza madawa ya binadamu na vifaa tiba nchini na kwa malipo ya awali ya asilimia 20 na nyingine inalipwa taratibu kwa makubaliano na Hospitali.
Ameongeza kuwa, Kas Medics imeanzisha mpango wa kutoa tuzo kwa wafanyakazi bora kwa Hospitali mbalimbali nchini ambazo zitakuwa zinatolewa kila baada ya miezi mitatu ili kutoa motisha kwa wafanyakazi wa afya kuwa na ari ya kuhudumia wateja kwa ufanisi zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Said Nkumba ambaye alikuwa mgeni rasmi amewataka wadau wa afya wanaojihusisha na usambazaji wa vifaa tiba na madawa nchini kuweka utaratibu wa kutoa motisha kwa watumishi bora wa sekta ya Afya wa serikali pia Wilayani humo badala ya kutoa kwenye hospitali binafisi pekee.

Mkuu wa Wilaya huyo ametoa akauli hiyo wakati akikabidhi zawadi kwa watumishi hodari wawili wa Hospitali ya Charles Kulwa (Memoriol) iliyopo katika kata ya Runzewe Wilayani humo zilizotolewa na Kas Medics kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo .

Said Nkumba amesema kuwa motisha kwa watumishi wa sekta ya Afya huchochea watumishi kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza bidii na weledi katika kuihudumia jamii na hivyo kuwaomba wadau hao kuweka utaratibu huo .

Nkumba alisema kuwa Afya ni sekta muhimu hapa Nchini katika kuihudumia jamii na kwamba serikali inatambua mchango mkubwa wa hospitali binafisi ambapo hosipitali ya kumbukumbu ya Charles Kulwa iimekuwa ni mkombozi mkubwa kutokana kutoa matibabu ya magonjwa mbalimbali .

Mkurugenzi Mtendaji wa hosptali hiyo Dkt. Baraka Charles alisema kuwa utaratibu wa kutoa motisha kwa watumishi wa Hospitali hiyo itakuwa mara nne kwa mwaka kwa kushirikiana na Kas Medics ili kuongeza utendaji bora kazin kwa watumishi hao wa kada ya afya .

Ameongeza kuwa Hospitali hiyo ilikuwa na utaratibu wa kutoa zawadi mara moja kwa mawaka lakini baada ya mpango wa washirika wao wa huduma za afyua Kas Medics kuja na mpango huo, sasa zawadi za wafanya kazi bora zitatolewa mara nne kwa mwaka.

Aidha Dkt Baraka amesema kuwa hospitali hiyo licha ya kutoa huduma za kawaida lakini pia inatoa matibabu ya kibingwa ikiwemo moyo, figo, masikio pamoja na matibabu ya magonjwa mbalimbali na huduma ya mama na mtoto.

Amesema kwasasa huduma za kibingwa zinazo tolewa katika Hospitali hiyo zimesaidia wagonjwa kutoka maeneo ya Kasulu,Kibondo,Ngara,Biharamulo,Muleba, Bukoba na Bukombe yenyewe.

Katika kutambua mfanyakazi bora katika Hospitali hiyo wafanyakazi wawili walipokea zawadi kutoka kwa KaS Medics ambao mmoja ni Mwanaume ambaye ni Emily Manyi na mwingine ni Mwanamke ambaye ni Dotto Biteko ambao walipokea zawadi ya vyeti pamoja ya fedha taslim.

Akisoma risala kwa mkuu wa Wilaya hiyo Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Mariana Bachilula amesema kuwa vigezo vilivyo tumika kuwapata wafanyakazi hao bora ni pamoja na tabia na mitazamo yao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Vigezo vingine ni idadi ya kesi za wagonjwa alizoona au kutatau,mahudurio katika wodi zao au idara ya kazi aliyopangiwa,namna anavyojali na kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na kutokuwa na makosa au kuwa nayo kwa uchache sana au kutolalamikiwa na wagonjwa juu ya huduma zake.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Said Nkumba (aliyeshika simu) ,Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya kumbukumbu ya Charles Kulwa Dkt. Baraka Charles (mwenye suti) na Mganga mkuu wa Hospitali hiyo Dkt.Mariana Bachilula wakiwa katika hafla ya kutangaza Mfanyakazi bora wa Hospitali hiyo. (Picha zote na Robert Kalokola/Diramakini Blog).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news