Waziri Kalemani azindua REA III Awamu ya Pili Mtwara

Na Veronica Simba – REA

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara unaolenga kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyosalia vya Mkoa huo.

Dkt. Kalemani alizindua Mradi huo Juni 19, 2021 katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Wabunge, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mjumbe wa Bodi hiyo Oswald Urasa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala, Mhandisi Jones Olotu pamoja na viongozi na wataalam mbalimbali wa Wizara, REA na TANESCO.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi, Waziri Kalemani alieleza kuwa lengo la Mradi husika ni kupeleka umeme katika vijiji 384 vya Mkoa wa Mtwara ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo.

“Mkoa wa Mtwara una vijiji vyenye umeme 413 kati ya 797. Kwa kutambua hilo, leo ninawakabidhi wakandarasi waushambulie mkoa huu kwa pamoja na kuhakikisha vijiji vyote vilivyosalia vinapatiwa umeme katika mradi huu,” alisema Waziri.

Alisema Mradi umefadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivyo akaishukuru Taasisi hiyo na kwa niaba ya Serikali akaahidi kuimarisha uhusiano mzuri baina ya pande hizo mbili.

Waziri Kalemani aliwataka wananchi wa Mtwara kuutumia umeme huo katika shughuli za kimaendeleo ili kuboresha maisha yao na hali ya kiuchumi ya nchi kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Kalolo alieleza kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeandaa Mpango Kazi wa Miaka Mitano uliojikita katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kusambaza nishati ya umeme katika vijiji vyote ifikapo Disemba 2022 na vitongoji vyote mwaka 2025.

Alisema kuwa Mpango Kazi huo ni wa miaka mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/26 na umejikita katika kufikisha umeme kwa Watanzania wote, maeneo ya viwanda, madini, kilimo, uvuvi na ufugaji.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakifurahi pamoja na vijana wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi Mtwara Vijijini, baada ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021. Wanafunzi hao walisema umeme utawawezesha kuongeza ufaulu katika masomo yao.

“Mheshimiwa Waziri, Mradi huu unaouzindua leo ni sehemu tu ya Mpango Mkakati wa Wakala na umelenga kusambaza umeme katika vijiji 1956 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme,” alibainisha.

Alieleza zaidi kuwa Mradi utatekelezwa katika mikoa 24 ambayo imegawanywa katika mafungu 39 na kwamba unakadiriwa kugharimu takribani shilingi trilioni 1.3 ambapo unatarajiwa kukamilika Disemba, 2022.

Wakili Kalolo aliongeza kuwa Mradi utakapokamilika utawezesha vijiji vyote 12,268 kupatiwa umeme na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kufikisha umeme katika vijiji vyote.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu akizungumza na wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala, alieleza kuwa katika Mradi huo mkoani Mtwara, wateja wa awali 6,182 wataunganishwa.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Mradi katika Mkoa huo utagharimu shilingi bilioni 62.146 ambapo utatekelezwa na Mkandarasi Namis Corporate Engineers and Contractors katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu na Mkandarasi Central Electricals Internationals katika Wilaya ya Mtwara Vijijini, Newala na Tandahimba.
Sehemu ya umati wa wananchi wakishangilia wakati wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.
Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakimpongeza Zairu Bakari, mwanafunzi wa Darasa la Pili, Shule ya Msingi Namtumbuka, ambaye alishiriki pamoja na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya, alisema umeme una umuhimu wa pekee katika Mkoa wa Mtwara kwani pamoja na kuwa ni fursa katika shughuli za kimaendeleo lakini pia ni muhimu kwa shughuli za kiusalama ikizingatiwa kuwa mkoa huo uko pembezoni mwa nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Wabunge wa Mtwara, Geofrey Mwambe (Ndanda), Issa Mchungahela (Lulindi), Katani Katani (Tandahimba), Hassan Mtenga (Mtwara Mjini) na Abdallah Chikota (Nanyamba) walipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu katika kuwapelekea wananchi wake maendeleo kupitia usambazaji umeme vijijini.
Mjumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Oswald Urasa akiwasalimu wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa tatu-kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mtwara, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara hiyo alipowasili mkoani humo kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Mtwara. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Namtumbuka, Mtwara Vijijini, Juni 19, 2021.

Aidha, wawakilishi hao wa wananchi waliipongeza Wizara ya Nishati, REA na TANESCO kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha Mtwara inafikiwa na umeme katika pande zote.

Waliwataka wakandarasi waliopewa dhamana ya kutekeleza Mradi husika kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa uaminifu na weledi huku wakiwahakikishia kuwa watawasimamia ipasavyo ili wasiiangushe Serikali na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news