Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ang'olewa, asisitiza watarudi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Utawala wa Muongo mmoja na nusu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu umeng'olewa rasmi nchini humo baada ya Bunge la taifa hilo ( Knesset) kupiga kura ya kuidhinisha serikali mpya ya muungano chini ya Naftali Bennett.
Benjamin Netanyahu ambaye ni komandoo wa kijeshi na mwanasiasa mahiri aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa tisa hadi 12 wa Israel kutoka 2009 hadi 2021 na hapo awali kutoka 1996 hadi 1999. Ingawa bado anaendelea kukiongoza Chama cha Likud na amesisitiza kuwa, siku za usoni wanarudi tena.

Naftali Bennett kutoka mrengo wa kulia tayari ameapishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Israel ambaye anachukua nafasi ya Netanyahu mwenye umri wa miaka 71.

Kwa hatua hiyo, Bennett ambaye ana umri wa miaka 49 ni mwanasiasa wa Israel ambaye anatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuendelea kuliongoza Taifa hilo na anakuwa Waziri Mkuu wa 13 kuanzia Juni 13, 2021 kupitia Chama cha Yamina.

Awali alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Diaspora kati ya mwaka 2013 hadi 2019 na mwaka 2019 hadi 2020 alihudumu kama Waziri wa Ulinzi nchini Israel.

Mheshimiwa Naftali Bennett kwa sasa ataongoza muungano wa vyama ulioidhinishwa kupitia uongozi mwembamba wa walio wengi wa 60 kwa 59 ambapo atahudumu kwa miaka miwili na nusu (kuanzia sasa hadi Septemba 2023).

Kupitia makubalino yao atamkabidhi nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu, Yair Lapid ambaye ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, kuongoza kwa miaka mingine miwili.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, pengine hii ni hatua nzuri kwa Mzee Netanyahu kwenda kukaa na familia yake kwa karibu chini ya mkewe Sara Netanyahu aliyemuoa mwaka 1991 baada ya kuachana na wake zake wawili akiwemo Fleur Cates aliyeishi naye mwaka 1981 hadi 1984 na Miriam Haran tangu mwaka 1972 hadi 1978.

"Kwa umri wake hana la kujutia wala kujiwazia mabaya, kwani amehudumu kwa muda mrefu kama mtumishi wa watu nchini Israel, hivyo ni wakati wake (Benjamin Netanyahu) kwenda kukaa karibu na familia yake chini ya mkewe wa sasa Bibi Sara ili waweze kuwalea kwa karibu zaidi watoto wao akiwemo Yair Netanyahu, Noa Netanyahu-Roth, Avner Netanyahu,"ameeleza Mchambuzi wa masuala ya Kimataifa katika mahojiano na DIRAMAKINI Blog.

Licha ya maoni hayo, Benjamin Netanyahu anatajwa kuwa miongoni mwa majasusi na wanasiasa wasiotabirika, kwani kwa mbinu alizonazo anaweza kurejea tena madarakani siku za usoni.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba, licha ya kushindwa sasa anakuwa ni Waziri Mkuu wa Israel aliyehudumu kwa miaka mingi na kiongozi wa kwanza kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu akiwa madarakani huku akishindwa kujinasua licha ya kutumia mbinu mbalimbali.

Changamoto za kufifisha juhudi zake za kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo zilianza kuonekana tangu mwaka 2019 baada ya kuitisha uchaguzi, lakini akashindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha ili kuunda serikali mpya ya muungano huku zikifuatia chaguzi zingine mbili ambazo zilifanyika bila mafanikio

Ndipo Disemba, mwaka jana ukafanyika uchaguzi wa nne ambapo licha ya ukubwa wa chama chake cha Likud katika Bunge la Taifa ambalo linaudwa na viti 120, malengo yake ya kuunda Serikali yalishindikana, hivyo Mheshimiwa Yair Lapid ambaye chama chake cha mrengo wa kati cha Yesh Atid kilikuwa cha pili kwa ukubwa akapewa nafasi.

Aidha, upinzani uliokuwa ukipinga utawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu madarakani uliongezeka hata kwa vyama vyenye msimamo sawa na chake.

Akiwa na msimamo mkali kuhusiana na jambo lolote linalohusiana na usalama wa Taifa la Israel, Benjamin Netanyahu ana historia ndefu ambapo mara zote amekuwa akijivunia kuwa, anaipenda Israel kwa kuwa ni mzalendo namba moja aliyezaliwa mjini Tel Aviv mwaka 1949.

Kwani hata pale ambapo mwaka 1963 familia yake ilihamia Marekani yeye Benjamin Netanyahu akiwa na umri wa miaka 18 alirejea nyumbani Israel na kujiunga na jeshi kwa miaka mitano alipohudumu kama nahodha katika kitengo cha juu cha makomando cha Sayeret Matkal nchini humo.

Maarufu kama Mfalme Bibi, alishiriki katika uvamizi wa uwanja wa ndege wa Beirut mwaka 1968 na kupigana vita mwaka 1973 vya Mashariki ya Kati.

Aidha, baada ya kuhudumu jeshini kwa muda, Benjamin Netanyahu alirejea nchini Marekani na kusomea Shahada na Shahada ya Uzamili katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts nchini humo.

Mwaka 1976, kaka yake Benjamin Netanyahu aliyefahamika kwa jina la Jonathan aliuawa na kusababisha uvamizi wa kuokoa wasafiri wa ndege waliokuwa wametekwa nyara na ndege ya Entebbe nchini Uganda.

Kifo hicho kiliibua hisia kubwa katika familia ya Netanyahau na jina lake likaanza kujulikana sana nchini Israel ambapo alianzisha taasisi ya kukabiliana na ugaidi kama kumbukumbu ya kaka yake.

Mwaka 1982 akiwa nchini Marekani alichaguliwa kuwa kiongozi katika ujumbe wa Israel mjini Washington DC, huku akifanya kazi zake kwa ufanisi hadi mwaka 1984 alipochaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa mjini New York. 

Hadi aliporejea nchini Israel mwaka 1988 na kujiingiza katika harakati za siasa kuanzia ubunge kupitia chama chake hadi nafasi yake ya Waziri Mkuu iliyofikia ukomo Juni 13, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news