Benki Kuu Tanzania yafungua ukurasa mpya mikopo, yalegeza masharti

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

BENKI kuu ya Tanzania ( BoT) imeanzisha mfuko maalum wenye thamani ya shilingi trilioni moja ambao utatumika kukopesha benki na taasisi za kifedha kwa riba ya asilimia tatu ili taasisi hizo ziweze kukopesha taasisi binafsi.

Akiongea na waandishi wa habari wakati akitoa hatua za kisera za upatikanaji wa mikopo binafsi na kupunguza viwango vya riba Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema, Benki au taasisi ya kifedha itakayofaidika na mfuko huo itakayotakiwa kukopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

"Hatua hii itaongeza ukwasi na kupunguza riba za mikopo kwa sekta binafsi," amesema Gavana huyo.

Aidha, amesema benki kuu imepunguza kiwango cha mtaji kitakachotumika kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo.

"Hatua hii itasaidia kutoa fursa kwa benki za biashara kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi kuliko ilivyokuwa hapo awali," amesema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Na kuongeza kusema kuwa, "Hatua hizi za kisera zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Sura. 197 na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa sura ya 437," amesema.

Hata hivyo, benki kuu imetoa unafuu kwa benki za biashara kwa kupunguza kiwango cha kisheria cha amana ambacho benki na taasisi za kifedha zinatakiwa kuweka benki kuu ikiwa ni sehemu ya kutekeleza sera ya fedha.

Amesema,mafuu hiyo itatolewa kwa benki itakayotoa mikopo kwa sekta ya kilimo kulingana na kiasi cha mkopo kitakachotolewa pia benki itakayonufaika itatakiwa kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

"Hatua hii inalenga kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo na kupunguza riba katika mikopo itakayotolewa, "amesema Gavana.

Pia ameeleza Benki Kuu ya Tanzania imeondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki.

Amebainisha kuwa, badala yake waombaji wa biashara ya wakala wa benki wanatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa au namba ya kitambulisho cha NIDA ambapo hatua hiyo itachangia kuongeza fedha katika benki kutokana na ongezeko la amana na kupunguza riba za mikopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news