Benki ya Mwalimu yatakiwa kuja na mikopo ya kuwanasua Walimu katika mikopo umiza

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

BENKI ya Mwalimu (MCB) imetakiwa kuja na njia bora itakayowasaidia walimu nchini kupata mikopo yenye masharti nafuu na kwa haraka ili kuwawezesha kuondokana na mikopo umiza.
Akiongea jijini Dodoma wakati alipokuwa akizindua bidhaa mpya ya mwalimu na ujasiriamali iliyoanzishwa na benki hiyo kwa ajili ya kukopesha mashine za uzalishaji mali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema, walimu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na aina ya mikopo wanayokopa kutoka katika taasisi ambazo zina masharti magumu na riba kubwa.

Amesema, hali hiyo imewafanya walimu kwa muda mrefu kukabiliwa na madeni kutoka taasisi hizo hali ambayo baadhi yao wanalazimika hata kuhama katika vituo vyao vya kazi.

“Lazima nyinyi kama Benki ya Mwalimu muangalie mnakuja kwa utofauti gani na taasisi nyingine za kifedha ili muweze kuwakopesha walimu wenye uhitaji fedha kwa ajili ya mambo mbalimbali yanayowakabili bila kuwapatia usumbufu," amesema Mtaka.

Pia, amesema kuwa imefikia hatua walimu wanakabidhi kadi zao za benki kwa taasisi za fedha na mishahara inapoingia tu kiasi chote cha fedha kinachukuliwa kwa makato.

Vile vile, amesema kuwa benki hiyo inatakiwa kujikita katika kuhakikisha kuwa inakuwa na kitu cha utofauti ambacho kitawavutia walimu na kujiunga nayo.

“Hili jina la Mwalimu benki mnaweza kuendelea nalo, lakini lazima muone kuwa utendaji wenu uwe kwa ajili ya makundi yote ili muweze kushindana na benki nyingine zaidi ya 50 zilizopo nchini,”amesema.

Aidha, amesema kuwa akiwa mkuu wa mkoa wa Simiyu alikuwa anapokea kesi nyingi za walimu kukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na madeni hali ambayo inaathiri taaluma katika mkoa husika.

“Kuna vituo vya kazi walimu hawafiki kwa kuhofia kuwa wanao wadai watakuja kudai mikopo yao tena unakuta mwalimu kakopa milioni mbili anakatwa milioni saba,”amesema.

Akizungumzia mpango huo wa mikopo ya mashine za uzalishaji mali amesema kuwa, ni ubunifu mzuri ambao kama utasimamiwa vizuri utawawezesha walimu kustaafu wakiwa na tabasamu.

Kadhalika, amewataka walimu kuchangamkia mkopo huo wa vifaa ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Richard Makungwa, amesema kuwa wamejikita katika kutoa huduma za kifedha kwenye ikolojia ya elimu ikiwa pamoja na vyuo vya elimu, walimu, shule, taasisi za elimu, wizara ya elimu na TAMISEMI.

“Mwalimu Commercial Bank iliandaa mkakati wa muda mrefu ukiwa na malengo ya kuboresha huduma zenye ubunifu katika kuwafikia wateja wetu,”amesema Makungwa.

Hata hivyo, amesema kuwa moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kuwa na bidhaa zinazolenga moja kwa moja mahitaji ya walimu katika kujiinua kiuchumi na kuleta tija kwenye jamii.

“Katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kukuza sekta ya viwanda na biashara na uchumi kwa ujumla Mwalimu benki tumeanzisha bidhaa mpya ya mwalimu na ujasiriamali ambayo inalenga kuwawezesha walimu, watumishi wa serikali pamoja na umma kwa ujumla kuwekeza, kukuza na kuwajengea uwezo kupitia shughuli za ujasiriamali ili kuwakwamua kiuchumi,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news