Dkt.Sengati:Wekeni wazee wasiojiweza katika mpango wa kunusuru kaya maskini, wapate bima iliyoboreshwa

Na Anthony Ishengoma, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati ameagiza TASAF Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha inawaweka wazee wote wasiokuwa na uwezo wanaingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini ili kupitia mpango huo waweze kupata katika Bima ya Afya ya Afya iliyoboreshwa.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Faustine Sengerema akiongea na baadhi ya Wazee hawapo pichani walioshiriki kikao cha Baraza hilo leo Mkoani Shinyanga.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema bado kuna wazee ambao bado wanafanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kunyanyaswa na kubaguliwa ikiwemo mauaji na kuendelea kuishi maisha magumu jambo ambalo linachangiwa na imani potofu katika jamii hivyo kuwataka vijana kuwalinda wazee hao ili waweze kuishi kwa amani kwani katika uzee binadamu anahitaji kupendwa.

Dkt. Sengati amesema hayo leo Julai 14, 2021 wakati wa ufunguzi wa kikao cha robo mwaka cha Baraza la Wazee wa Mkoa wa Shinyanga na kuikumbusha jamii kutambua kuwa kadili mwili wa binadamu unavyozeeka ndivyo viungo vinavyochoka hivyo kufanya wazee kupata magonjwa nyemelezi kama vile kisukari, presha na magonjwa mengine.

Dkt.Sengati ameongeza kuwa, mkoa wake una jumla ya wazee 66,717 ambao kati yao wanaume ni 29,717 na wanawake 36,500 na kati ya hao wazee wenye Bima ya Afya iliyoboreshwa 20,545 akiitaja idadi hiyo kuwa ndogo sana ukilinganisha na idadi wazee iliyopo katika mkoa wa Shinyanga na kutaka watendaji kuendelea kuimiza wazee kujiunga na Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu.
Baadhi ya Wazee walioshiriki kikao cha Baraza la Wazee cha Mkoa wa Shinyanga wakisoma dua kabla ya kuanza kikao chao leo leo Mkoani Shinyanga.

Naye Mzee Anderson Lymo Katibu wa Wazee Mkoa wa Shinyanga amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuangalia zaidi suala la matibabu ya wazee kwa kuwa suala la ukosefu wa dawa kwa ajili ya matibabu ya wazee katika vituo vya afya bado ni changamoto kubwa kwa wazee hapa nchini.

Mzee Lymo ameongeza kuwa, pamoja na upatikanaji wa bima za afya kwa wazee haitoshi kwani changamoto iliyopo imekuwa ni upatikanaji wa madawa katika zahanati, vituo vya afya na hata hospitali kubwa na changamoto kubwa zaidi inayowakumba wazee ni umasikini kwakuwa wengi hawana shughuli inayowapatia kipato.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga, Mzee Faustine Sengerema amemuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati suala la wazee kushirikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo serikali za vijiji na maeneo mengine ili kuwawezesha wazee kupaza sauti na kutoa ushauri kwa maendeleo ya Taifa.
Viongozi wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga wakishiriki sala kabla ya kuanza kikao chao leo Mkoani Shinyanga.

Mzee Sengerema amesema kuwa, suala la wazee kushirika katika maamuzi mbalimbali linatokana na miongozo mbalimbali iliyopo, lakini utekelezaji wake umekuwa haufanyiki hivyo kuwanyima wazee haki ya kushirikishwa katika masuala mbalimbali ya mustakabali wa nchi.

Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga linakaa kwa siku moja kufanya kikao chake cha robo mwaka ikiwemo maandalizi ya uchaguzi wa baraza jipya la wazee ambalo lina wawakilishi kutoka halmashauri zote sita zinazounda Mkoa wa Shinyanga na mabaraza mengine kama hayo tayari yameundwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news