Freeman Mbowe apelekwa Segerea kwa kukosa dhamana

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mawili yanayomkabili likiwemo la ugaidi.

Mbowe amefikishwa katika Mahakama hiyo leo Julai 26, 2021 na kusomewa mashataka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin akisaidiana na Tulimanywa Majigo alidai kuwa,  Mbowe anaunganishwa na washtakiwa wengine watatu waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka mengine yote ya ugaidi wanayodaiwa kuyatenda mwaka 2020.

Katika kosa la kwanza Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa ambapo anadaiwa kula njama hiyo kati ya Mei na Agosti 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.

Baada ya kusomewa maelezo Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka, kesi imeahirishwa hadi Agosti 5, 2021 na upelelezi umekamilika ambapo zinasubiriwa nyaraka ili ihamishiwe Mahakama Kuu. 

Wiki iliyopita Jeshi la Polisi nchini lilithibitisha kumshikilia Mbowe kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo ugaidi.

Haya hivyo, baada ya kusomewa mashtaka, Mbowe amepelekwa katika gereza la Segerea baada ya kukosa dhamana.

Awali Chama Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kililitaka Jeshi la Polisi kumpeleka hospitali mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ili kupatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Julai 26, 2021 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema imeeleza kuwa walipokea taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia ambao walimtembelea asubuhi katika kituo cha polisi Osterbay.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news