Jukwaa la Wahariri lamshukia Msemaji wa Simba SC, Haji Manara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesikitika na kulaani kitendo cha msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara kumdhalilisha mwandishi wa Habari wa Redio Clouds FM, Prisca Kishamba.
Taarifa iliyotolewa na jukwaa hilo leo Ijumaa Julai 2, 2021 na mwenyekiti wake, Deodatus Balile inaeleza kuwa udhalilishaji huo ulioambatana na maneno ya kashfa ulifanywa kwenye mkutano wa Simba na waandishi wa habari uliofanyika Juni 30, 2021 mkoani Dar es Salaam.

TEF imemtaka Manara kuacha mara moja tabia ya kutumia mikutano ya klabu ya Simba na hata mitandao ya kijamii kuwadhalilisha wanahabari.

Limesema ikiwa kuna suala lolote ambalo mwandishi wa habari amelitenda kinyume cha maadili na miongozo ya taaluma, wahusika wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwa taasisi za kihabari au kwa mwajiri wa mwandishi husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Kupitia taarifa hiyo, TEF imeuomba uongozi wa timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumuonya Manara kuacha tabia hizo mara moja kwani hazina afya na haziongezi thamani yoyote kwa Simba wala taaluma ya habari.

“Ikiwa vitendo vya aina hii vitaendelea kujitokeza, TEF kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari na vyombo vya habari hatutakuwa na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua zaidi Ili kuwaepusha waandishi wetu dhidi ya unyanyaswaji na udhalilishwaji.

“Kauli za vitisho vya Manara ni mwendelezo wa tabia na mwenendo wake dhidi ya waandishi wa habari ambao wamekuwa wakiripoti habari za Simba kwa maslahi mapana ya umma na sekta ya michezo kwa ujumla,” inaeleza taarifa hiyo.




Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news