Katibu UWT Longido: Mwelekeo wa Rais Samia unatupa heshima wanawake na Taifa letu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KATIBU wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Judith Laizer amepongeza mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akisisitiza kuwa, umoja huo utaendelea kusimamia imara kumtetea na kuunga mkono juhudi zake za kuwaletea maendeleo Watanzania.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele katika kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia na utawala bora, hivyo anaamini kasi yake itawezesha maendeleo kuimarika kwa haraka hapa nchini.
Ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumzia Siku 100 za Uongozi wa Rais Samia tangu aapishwe Mei 19,mwaka huu.

Katibu huyo wa UWT amesema kuwa, Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi CCM kwa kuzingatia ushirikiano na ujumuishi wa makundi mbalimbali.

Amesema, katika siku 100, Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha mwelekeo mzuri katika kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia.

“Kila mmoja wetu anatambua wazi kuwa, suala la jinsia ni suala la maendeleo,ni suala la uchumi, ni suala la kila kitu, hivyo ni lazima lipewe kipaumbele.

"Mara nyingi tumeona uchumi umekuwa ukiyumba kutokana na masuala ya kijinsia kutopewa uzito. Tunatarajia kwa mwelekeo huu tunaokwenda nao katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mbali na kuimarika kwa usawa katika nyanja mbalimbali maendeleo yetu nayo yatakwenda kwa kasi sana,"amesema Laizer.

Amesema, anampongeza Rais Samia kwa kuthamini na kuupa kuyapa kipaumbele masuala ya usawa wa kijinsia kwenye uongozi, kwani ni kitu ambacho kimezungumzwa kwa muda mrefu tangu mkutano wa Beijing.

Sambamba na utekelezaji wa Azimio la Beijing ambapo awamu zilizopita zilifanya juhudi zake,lakini kupitia awamu hii chini ya Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na juhudi ambazo ni tofauti.

"Juhudi hizi kwa kweli tunaona zitatusogeza mbele zaidi, kwa kweli ninafarijika sana kuona Mkuu wa nchi anazungumza wazi wazi kwamba kwenye masuala ya uongozi atatoa kipaumbele pia kwa wanawake wenye uwezo.

"Kila mmoja wetu tayari ameona Mheshimiwa Rais anachofanya, kwa upande wa makatibu tawala ameteua wanawake asilimia 48, hii inakuwa ni kwa mara ya kwanza.

"Pia hiki ni kitu cha kujivunia, si tu na Watanzania bali Dunia nzima,”amesema Judith Laizer.

Aliongeza kuwa, “Hizi siku 100 ni za kusherehekea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amelipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia.

"Tumeona pia Mheshimiwa Rais ameteua majaji wanawake asilimia 42.8, mabalozi asilimia 33.3 lakini pia wakuu wa wilaya asilimia 31. Hii ni hatua njema na ya kupongeza sana,”amesema.

Laizer amesema, kutokana na hali hiyo kwa sasa mwendo uliopo ni wa tofauti, mambo yanaenda vizuri kinachotakiwa ni kutoa ushirikiano, wale waliochaguliwa na kuteuliwa waendelee kujitoa, wafanye kazi vizuri, kwa uaminifu, uadilifu ili kuonesha kwa vitendo kuwa wanawake wana uwezo wa ziada katika kusaidia uharakishaji wa maendeleo nchini.

Pia amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kuonesha mabadiliko kwa kuangalia tunu za kuongoza taifa.

Miongoni mwa mambo hayo, Laizer amesema ni masuala ya haki, kilimo chenye tija, demokrasia, usawa na uhuru wa vyombo vya habari, kuondoa umaskini na rushwa ikiwemo ubadhirifu wa mali za umma na ukusanyaji kodi usio na bughudha katika nyanja mbalimbali.

Aidha, kuhusu mageuzi ya kilimo ambapo mkulima mdogo, mwanamke ndiyo amebeba taifa katika uhakika wa chakula, Judith Laizer alishauri mwanamke asije akatupwa pembeni.

Katibu huyo wa UWT wilayani Longido amesema, kuwe na mikakati mahususi ili kuhakikisha kuna ushiriki wa wakulima wadogo wadogo hususani wanawake waliopo kwenye maeneo ya pembezoni hasa vijijini ambao wamekuwa wakiteseka kila siku.

Laizer ameshauri wanawake wapewe kipaumbele zaidi kwenye elimu ya ujuzi kwenye vyuo vya ufundi ambavyo vipo maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema kuwa, anaamini katika masuala yote yanayopewa kipaumbele ikiwemo maji, afya, elimu, madini, viwanda, Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), madini na vingine wanawake nao watakuwa wanufaika wa vipaumbele hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news