Kilio cha tozo za miamala chatua kwa Rais Samia, Waziri Mwigulu atoa neno

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Siku chache baada ya malalamiko kuzuka kila kona ya nchi kutoka kwa wananchi kutokana na maumivu wanayoyapata katika tozo za miamala wanayoifanya kwa kutuma au kutoa fedha, hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesikia kilio hicho.
Hayo yamethibitishwa leo Julai 19, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba.

"Mheshimiwa Rais naye ameguswa na jambo hili, amesikia maoni ya Watanzania wote, ameshatoa maelekezo kwamba tuyafanyie kazi haya malalamiko ambayo wananchi wanayatoa.TAZAMA VIDEO 📸 

"Nitoe rai kwa wananchi kuwa Serikali imesikia malalamiko ya wananchi na tayari tumeendelea kuyafanyia kazi, Waziri Mkuu ameshaitisha kikao kesho kuendelea kupitia masuala haya haya.

"Kwa sababu hii ni sheria ya Bunge, na tayari imeshapitishwa na inatakiwa kutekelezwa, lakini kuna maeneo ambayo yanaangukia kwenye kanuni ambazo zinaangukia Wizara ya Fedha na Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano,"amesema Waziri huyo.

Awali DIRAMAKINI Blog ilifanya mahojiano na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph ambapo alionyesha kuguswa na maumivu ya tozo hizo huku akimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutumia hekima na busara zake kuwaokoa Watanzania wanyonge katika tozo kubwa za miamala ya simu.
"Awali ya yote nichukue nafasi hii kumuomba sana...sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuangalia upya namna ambavyo Serikali yake itafanya ili kuwaokoa wanyonge hasa katika tozo za miamala ya simu.

"Kwani tozo hizo ambazo zilianza kukatwa kupitia miamala mbalimbali inayofanyika kupitia kampuni za simu tangu Julai 15, mwaka huu zimekuwa za kiwango cha juu sana.

"Ni tozo ambazo zinatoa maswali mengi baada ya kupendekezwa na Wizara ya Fedha na Mipango na hatimaye kupitishwa rasmi katika Bunge la bajeti ambalo limemalizika karibuni. Kwa haraka haraka, tozo hiyo imewaongezea mzigo wananchi katika gharama za uendeshaji wa maisha ya kila siku maana wananchi wanyonge hutegemea simu kufanya miamala katika shughuli zao za kila siku, kama vile biashara hivyo kutokana hali hivyo itasababisha faida kupungua katika biashara.

"Na inaweza kusababisha mzunguko wa fedha kupungua kwa wananchi, hivyo na kuleta mdororo wa kiuchumi kwa wananchi,pia wananchi wanyonge watapoteza ajira, kwani wengi walikuwa wamejiari kwa kufanya biashara hivyo inaweza kupunguza watumiaji kwa kuamia njia zingine,hii ni kutokana na makato makubwa ya kutoa na kutuma pesa,"amesema Mwalimu Makuru.Endelea hapa;Mwalimu Makuru amuangukia Rais Samia kuhusu tozo za miamala ya simu "HUU NI MTEGO KWA CCM"

Post a Comment

0 Comments