Kwikwi yamtesa Rais Bolsonaro akimbizwa hospitalini Sao Paulo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amepelekwa kwenye Hospitali ya Sao Paulo ambako huenda akafanyiwa upasuaji.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais imeeleza kuwa, Rais Bolsonaro amekuwa akisumbuliwa na kwikwi kwa siku 10 mfululizo ambapo madaktari wamesema aligundulika na matatizo kwenye utumbo.

Rais Bolsonaro mwenye umri wa miaka 66, alitakiwa kuwa chini ya uangalizi wa madaktari nyumbani au hospitali kwa muda wa saa 24 au 48.

Aidha,taarifa hali ya kiafya ya Bolsonaro imezusha maswali mengi kutokana na kusumbuliwa pia na kifua cha mara kwa mara kufuatia kuambukizwa virusi vya corona (COVID-19) mwaka 2020.

Hata hivyo, Rais Bolsonaro amefanyiwa upasuaji kadhaa baada ya kuchomwa kisu tumboni wakati wa kampeni za urais mwaka 2018.

Bolsonaro ambaye amewahi kuwa mbunge na afisa mstaafu wa jeshi, mwaka huo alikimbizwa hospitalini mjini Sao Paulo kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya haraka baada ya kuchomwa kisu hicho akiendelea na kampeni mjini Juiz de Fora.

Mshukiwa alikamatwa wakati wa shambulio hilo na aliwaambia polisi kwamba alikuwa akitimiza ujumbe aliopewa na mungu.

Rais Jair Bolsonaro akiwapungia mkono wananchi mjini Rio de Janeiro hivi karibuni. (Picha na Silvia Izquierdo/AP/ Diramakini Blog).

Post a Comment

0 Comments