Maafisa TRA, polisi ni miongoni mwa waliodakwa wakiuza Heroin kilo 99 Dar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imefanikiwa kukamata kilo 99.33 za dawa za kulevya katika matukio ambayo yanawahusisha watuhumiwa nane ambapo kati yao watatu ni watumishi wa Serikali.

Watuhumiwa watatu ambao ni watumishi wa Serikali ni pamoja na Ofisa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Andrew Paul (45) mkazi wa Kurasini, Askari Polisi F.6763 CPL Deodatus Massare (37) pamoja Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ally Juma Ally(32) mkazi wa Kinyerezi.

Kwa upande wake watuhumiwa wengine ni pamoja na Mariami Bacha (28) na mumewe Jamal Nangatukile (45), Said Mgoha (46), George Mwakang'ata(38) pamoja na Abubakar Abdall(28).
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam leo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya wakati akitoa tathimini ya operesheni ya ukamataji wa dawa za kulevya kwa kipindi cha mwezi Juni amesema, watuhumiwa hao walitiwa mbaroni na mamlaka hiyo baada ya kufanya uchuguzi na kugundua wanajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Amesema Juni 18, mwaka huu katika eneo la Mburahati Madoto mkoani Dar es Salaam, DCEA ilifanikiwa kumkamata mume na mke ambao ni Jamal Nangatukile na mkewe Mariyamu Bacha wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 494.52 .

Kamishina Jenerali Kusaya aliendelea kueleza kuwa, Juni 19 katika eneo la Bunju Beach, mamlaka hiyo pia ilifanikiwa kumkamata aliyekuwa Askari Polisi F.6763 CP Deodatus Massare akiwa na kilo 1.04 ya dawa za kulevya aina ya heroin.

Pia katika maeneo ya Mivijeni mkoani Dar es Salaam, Juni 21 mwaka huu walimkamata Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Andrew Paul mkazi wa Kurasini ambaye alikuwa na wenzake Said Mgoha maarufu kama Kidimu mkazi wa Mtoni Kijichi pamoja na George Mwakang'ata wakiwa na dawa za kulevya aina heroin kiasi cha kilo 1.02

Katika eneo jingine Juni 23, mwaka huu mamlaka hiyo imefanikiwa kumkamata Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ally Juma Ally akiwa na mwenzake, Abubakar Abdall wakiwa na dawa za kulevya aina Methamphetamine zenye uzito wa gramu 597.61 ambapo katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwake maeneo ya Zimbi Kinyerezi kuliweza kupatika pesa taslimu kiasi cha shilingi milioni 82 .43 pamoja na dola za kimarekani 5100.

Kamishina Jenerali Kusaya amesema, watuhumiwa wote tayari wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya kujihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.

"Makosa yote waliyokutwa nayo watuhumiwa hawa ni ya uhujumu uchumi kwa Sheria ya nchi yetu pamoja na hatua tulizofikia bado tunaendelea na uchuguzi ili kuwabaini wahalifu wengine walioshiriki katika tukio hilo,"amesema.

Hata hivyo, Kamishina Jenerali Kusaya ametoa ovyo kali kwa wale wote wanaotaka kujaribu makali ya Serikali kwa kuendelea kujihusisha na hiashara haramu ambapo amewataka kuacha mara moja na watafute kazi nyingine halali ya kupata kupato.

"Ninawaonya watu wote wanaojihusisha na biashara hii haramu ya dawa za kulevya, wanapaswa kuacha mara moja kwani DCEA tupo macho usiku na mchana, tutawakamata katika siku wasiyoijua na kuwawajibishwa kwa mujibu wa sheria,"amesisitiza Kamishina Jenerali Kusaya.

Aidha, ameiomba jamii kwa ujumla kuendelea kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa mtu au kundi la watu linapojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya huku akisisitiza kuwa janga hilo lisiposhughulikiwa katika umoja litaua nguvu kazi ya Taifa.

Kamishina Jenerali Kusaya amewaomba waandishi wa habari kuendelea kutumia kalamu kuwapa elimu watanzania na jamii kwa ujumla juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine Kamishina Jenerali Kusaya amesema toka ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu kipindi cha miezi mitatu amefanikiwa kukamata jumla ya kilo 953.

Amesema, lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha wanatokomeza mtandao wa biashara haramu ya dawa za kulevya kutokana na kuua nguvu kazi ya Taifa.

Pia amebainisha kuwa, nguvu ya Taifa ambayo ni kuanzia vijana wa umri wa miaka 15 hadi 40 imekuwa ikiangukia katika wimbi hatari la mtandao wa dawa za kulevya na kupelekea kuwa waraibu.

Post a Comment

0 Comments