Mbunge Mtenga akabidhi matofali Shule ya Mitengo, atoa ombi TARURA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MBUNGE wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga ameendelea kutekeleza ahadi mbalimbali ambazo alizitoa wakati akiomba ridhaa ya wananchi wa jimbo hilo kwenda kuwawakilisha bungeni.

Kupitia mfuko wa jimbo hilo, Mbunge Mtenga juzi amekabidhi matofali 1,000 yenye thamani ya shilingi 1,000,000 katika Shule ya Msingi Mitengo iliyopo Kata ya Mitengo Manispaa ya Mtwara Mikindani ili kuendeleza ujenzi wa vyumba mitatu vya madarasa katika shule hiyo.
Pamoja na matofali hayo, Mtenga ameahidi kuwaongezea matofali, mabati pamoja na saruji mifuko 40 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.

Aidha katika kuunga mkono juhudi za Serikali,Mbunge Mtenga amewataka wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuendelea kujitoa na kushirikiana na Serikali ili kuboresha Sekta ya Elimu kwa manufaa ya watoto wote.

Wakati huo huo, Mbunge Mtenga ameutaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini Manispaa ya Mtwara-Mikindani (TARURA) kujenga barabara za lami maeneo ya Pembezoni mwa Mji ili kuwaondolea adha wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Amesema kuwa, barabara nyingi katika maeneo hayo zimekuwa zikiharibiwa na mvua mara kwa mara na kuwafanya wananchi katika kupata changamoto ya usafiri pindi wanapotaka kwenda mjini kupata mahitaji mbalimbali.

Mbunge Mtenga aliyasema hayo Julai 10, mwaka huu alipofanya ziara ya ukaguzi wa barabara zinazoendelea kutengenezwa katika maeneo mbalimbali.

Pia aliwapongeza TARURA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuimarisha miundombinu ya barabara kwa sasa kwa kuwa maeneo mengi yanapitika kwa urahisi.

Akijibu hoja ya Mbunge Mtenga, Meneja wa TARURA Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mhandisi Hatibu Nunu amesema kuwa katika bajeti ya 2021/2022 iliyoanza Julai wametenga shilingi milioni 990 kwa ajili ya kuboresha barabara ya Nkanaredi yenye urefu wa kilomita 1.2 inayoanza Stendi ya Mabasi hadi Mnjaleni shilingi milioni 490 na barabara ya Mangamba chini hadi Nazareti yenye urefu wa mita 650 shilingi milioni 500 na zote zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema kuwa, mradi wa ujenzi wa barabara ya Nkanredi usanifu umeshakamilika na tenda ya ujenzi wa barabara itatangazwa hivi karibuni wakati barabara ya Mangamba Chini usanifu wa awali umeshafanyika na taratibu zingine zinaendelea.

Barabara nyingine zitakazojengwa kwa kiwango cha lami katika bajeti 2021/2022 ni pamoja na barabara ya Kawawa, Mkwawa na Mkoani zilizopo Kata ya Rahaleo zenye urefu wa kilomita 1.2 zitakazogharimu shilingi milioni 600.

Post a Comment

0 Comments