Milioni 520/- za Bima ya Afya kupitia NHIF zapigwa, KCMC, Mawenzi watajwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kupitia ukaguzi maalumu unaoendelea kufanyika katika miamala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) umebaini kuwepo kwa ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 520 mkoani Kilimanjaro.

Wizi huo unaohusisha watumishi sita wakiwemo kutoka na hospitali za rufaa ya Kanda KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi.
Imebainika kuwa, KCMC wanaongoza kwa ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 245 kwa kugushi nyaraka na kujipatia fedha hizo kinyume na sheria.

Akizungumza baada ya kikao kazi na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo wakuu wa hospitali za KCMC, Mawenzi na wale wa bima ya afya, Naibu Waziri wa Afya, Dkt.Godwin Mollel amesema kutokana na tuhuma za kuwapo kwa udanganyifu huo anataka hatua za kinidhamu na sheria kuchukuliwa.

Amesema, ubadhirifu huo umefanywa na baadhi ya watumishi kwa kushirikiana na baadhi ya maduka ya dawa za binadamu ambayo uchunguzi unaendelea kubaini zaidi.

Dkt.Mollel amesema, Serikali itakwenda mikoa yote nchini ili kufanya uchunguzi huo na kwamba wapo baadhi ya watumishi wamekiri kuhusika na udanganyifu huo na wameanza kurejesha fedha walizojipatia.

"Uchunguzi wa awali umebaini wapo madaktari na wauguzi wasio waaminifu ambao kwa makusudi wanatumia kadi za wateja na kushirikiana na maduka ya dawa yanayotumia NHIF kughushi matibabu hayo na kujilipa fedha hizo," amesema.

Aidha, Naibu Waziri amezitaka taasisi na maduka yanatoa huduma za afya kujaza fomu za bima za afya kwa madai halali na kila mtanzania kuhakikisha kadi yake ya afya inatumika kufanya malipo halali.

Pia amewataka wote wenye nia ya kufanya ubadhirifu wowote kuacha mara moja kwani lazima watajulikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani bado uchunguzi unaendelea na unafanyika katika mikoa yote nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameviagiza vyombo vya usalama kuwakamata wote waliohusika nakuchukuliwa hatua za kisheria pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani kupitia bajeti ya mwaka huu 2021 imetenga kiasi cha zaidi ya sh.Bilioni 148 kwa ajili ya kupeleka katika mfuko wa bima ya afya kwenda kusadia wananchi maskini na wasiojiweza,"amesema.

RC Kagaigai amewataka watumishi wa umma kuwa waaminifu kwani fedha za serikali zimelenga kuwasaidia Watanzania wote nchini.

Post a Comment

0 Comments