NAIBU WAZIRI MABULA KUSIKILIZA MIGOGORO YA ARDHI MASASI

Na Munir Shemweta, MASASI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maenedeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula atasikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za ardhi katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kwa siku mbili kuanzia Jumanne tarehe 27- 28 Julai mwaka huu.  

Hatua hiyo inafuatia kujitokeza kwa changamoto za ardhi wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Isdor Mpango wilayani Masasi mkoa wa Mtwara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Mendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula.

Wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika uwekeji jiwe la msingi katika soko la Kisasa la Jidah lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi Julai 25, 2021, Dkt.Mpango aliwaita Mawaziri alioambatana nao ili waeleze mikakati ya wizara zao katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za masuala mbalimbali.

Akielezea mikakati ya wizara yake kuhusiana na changamoto za migogoro ya ardhi kwenye wilaya hiyo ukiwemo mgogoro baina ya Jeshi la Magereza na Wananchi wa Kata ya Namajani kuhusiana na fidia, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula alisema, suala la fidia katika mgogoro huo liko katika mazungumzo kuhakikisha suluhu inapatikana kwa katika kipindi cha muda mfupi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwasili kata ya Jida kuweka jiwe la msingi Soko la wafanyabiashara ndogondogo la Jidah lililopo Wilaya ya Masasi.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, migogoro ya ardhi ipo mingi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ile ya wilayani Masasi na kubainisha kuwa, migogoro hiyo isiposimamiwa kwa wakati inaweza kuleta shida kubwa kwa wananchi.  

Alisema, Wizara yake imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua kama siyo kuisha kabisa katika maeneo mbalimbali nchini na moja ya jitihada hizo ni kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na kumilikishwa.
 
Naibu Waziri Dkt. Mabula alisema, jumanne tarehe 27 hadi 28 Julai 2021 atasikiliza na kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya wilayani Masasi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea maelezo kutoka kwa Leonard Mkondola ambaye ni Fundi Mchundo wa soko la kisasa la Jida mara baada ya kuwasili kuweka jiwe la msingi sokoni hapo.

“Mhe. Makamu wa Rais hapa Masasi kuna migogoro ya ardhi, nafahamu upo mgogoro kati ya jeshi la Magereza na wananchi wa kata ya Namajani kuhusu fidia, wakati nakuja kuzindua nyumba za makazi za NHC jumanne nitakaa hapa Masasi na kuzipatia ufumbuzi changamoto za ardhi,” amesema Dkt.Mabula. 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula yuko kwenye msafara wa ziara na Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango mkoani Mtwara ambapo tarehe 26 Julai 2021 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataweka jiwe la Msingi kwenye Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo liko chini ya Wizara ya Ardhi.

Post a Comment

0 Comments