PASS kuwawezesha wakulima kupata mikopo zana za kilimo bila dhamana

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Kampuni mpya ya PASS Leasing inayomilikiwa na Taasisi ya PASS Trust itaanza kutoa mikopo ya zana za kilimo kwa wakulima wadogo, kati na wakubwa na vikundi vinavyojishughulisha zinazoendana na kilimo bila dhamana yoyote.
Kaimu Mkurugenzi wa PASS Trust, Anna Shanalingigwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri.

Akizungumza jijini leo Julai 21, 2021 jijini Dodoma kuhusu Wiki ya Pass Trust itakayofanyika kati ya Julai 22 hadi 24, mwaka huu jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya PASS Trust, Annah Shanalingigwa amesema, mikopo hiyo ya zana za kilimo inalenga kuwezesha wakulima kumiliki vifaa hivyo bila kuweka dhamana yoyote.

"Mikopo hiyo bila dhamana inalenga kuwezesha shughuli za kilimo katika mnyororo mzima wa thamani, kuweza kumiliki vifaa hivi bila kuweka dhamana yoyote kama ilivyozoeleka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha," amesema.

Kampuni ya Pass Leasing ambayo tayari imeanza kutoa huduma za mikopo ya zana za kilimo unawawezesha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa na vikundi mbalimbali inawaalika wakulima, wafugaji na wavuvi na wajasiriamali katika mnyororo mzima wa thamani kufika Nyerere Square kukutana na wadau ili kuwezeshwa upatikanaji wa mitaji kupitia udhamini wa Pass Trust na piankutapa suluhu ya changamoto zinazotokana na upatikanaji wa fedha hizo.

Taasisi ya Pass Trust kupitia kaulimbiu, 'Pamoja tunaweza upatikanaji wa fedha kwa kilimo endelevu,' itatumia nafasi hiyo kuzungumza na wadau wa kilimo kuhusu upatikanaji wa fedha za kuchochea ukuaji wa kilimo biashara nchini.

Lengo la Pass Trust ni kuwaleta pamoja wadau wao wakiwemo wakulima, wauzaji wa zana za kilimo, taasisi za fedha, wauza pembejeo, viongozi wa serikali, wachakataji ili kuzungumzia masuala ya upatikanaji wa fedha kama kuchocheo cha ukuaji wa kilimo biashara.

Pass Trust tangu kuanzishwa na Serikali na Denmark miaka 20 iliyopita kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha na biashara kwa wajasiriamali wa sekta ya kilimo, imekuwa ikitoa dhamana ya mikopo kati ya asilimia 20-60 na hadi 80 kwa wanawake kwa benki shirika.

Tangu mwaka 2000 taasisi hiyo ilipoanzishwa imeshadhamini takribani miradi 46,300 yenye thamani ya shilingi trilioni moja ambapo takribani wajasiriamali milioni 1.7 ambapo asilimia 45 ni wanawake wamenufaika na udhamini huo.

Pass Trust kupitia udhamini wa miradi hiyo na kunufaisha wajasiliamali hao, vile vile imetengeneza ajira milioni mbili na nusu ambazo zimeboresha maisha ya Watanzania.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema, katika wiki hiyo imeandaa programu pia katika kanda ya Mashariki na Pwani ambapo Julai 22 viongozi wa taasisi watakuwa Singida na Julai 28 watakuwa Mafia mkoani Pwani na Zanzibar watakuwa Julai 31, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akizungumza katika mkutano huo aliipongeza Taasisi ya PASS Trust kuamua kufanya Wiki ya Taasisi mkoani humo ili kuwezesha wadau wa sekta ya kilimo kupata mikopo ya zana za kilimo bila dhamana.

Shekimweri alisema, kwa kutoa mikopo hiyo, itasaidia wananchi wengi kujikita katika kuzalisha mazao mbalimbali hasa zabibu ambalo ni zao mkakati la mkoa wa Dodoma.

Mkuu huyo amesema kwa kusaidia mikopo ili kuwezesha wakulima kupitia Kampuni Hodhi hiyo ya PASS Leasing kunaenda sambamba na Ilani ya CCM inayotaka kufanyika mapinduzi katika kilimo kuacha kutumia kilimo cha jembe la mikono na kutumia zana za kisasa na kuachana na ufugaji holela na kufuga kisasa.

Wiki ya Pass Trust ilioandaliwa kwa ushirikiano na Hamshauri ya Jiji la Dodoma inazinduliwa leo Julai 22 mwaka huu na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na itafungwa na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda Julai 24, mwaka huu ambaye pia atazindua kampuni tanzu ya Pass Leasing.

Post a Comment

0 Comments