Polisi auawa saa tano usiku akijaribu kumkamata mwizi wa mazao Arusha

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Askari wa Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha polisi Mbuguni wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha ameuawa kwa kukatwa na panga kichwani wakati akijaribu kumkamata mtuhumiwa wa wizi.

Tukio hilo limetokea Julai 23,2021 majira ya saa tano usiku katika Kijiji cha Makiba wakati askari huyo ( jina linahifadhiwa) alipoenda nyumbani kwa mhalifu kwa lengo la kumkamata.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP-Justine Masejo amesema, askari huyo alifariki dunia muda mfupi baada ya kuvunja damu nyingi.

"Askari wetu katika kituo kidogo cha polisi Mbuguni alikatwa panga kichwani na kufariki dunia baada ya kwenda nyumbani kwa mhalifu majira ya saa tano usiku,kwa lengo la kumkamata, sasa polisi wanaendesha operesheni ya kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya dola,"amesema.

Amefafanua kwamba, askari huyo alienda nyumbani kwa mtuhumiwa kwa nia ya kumkamata kuhusiana na matukio ya wizi wa mazao na kwamba wakati akijaribu kumkamata ndipo alipotokea mhalifu mwingine nyumba ya jirani ambaye alimkata panga moja kichwani askari huyo..

Kamanda Masejo ameongeza kuwa, kabla ya tukio hilo mwananchi mmoja alifika katika kituo cha polisi Mbuguni kulala juu ya mtuhumiwa wa wizi wa mazao yake ambapo polisi walianza msako wa kumvizia mtuhumiwa huyo.

Amesema kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa uchunguzi, aliweza kufanikiwa kutoroka baada ya tukio hilo na polisi wameanzisha msako mkali.

Post a Comment

0 Comments