Rais Dkt.Mwinyi apokea taarifa ya utafiti unaolenga kuinua uchumi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Taasisi ya “The Brent Hust Foundation” kwa kufanya kazi nzuri ya utafiti unaohusu upangaji na utekelezaji wa mipango na Sera za kiuchumi kwa maendeleo ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizindua Kitabu cha Rais mstaafu wa Nigeria, Mhe. Obasanjo “Asian Aspiration“ uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni jijini Zanzibar na kulia kwake ni Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe Olusegun Obasanjo na kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, lengo la taasisi hiyo kufanya utafiti ni kuweza kushirikiana vizuri na Serikiali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala mbalimbali ya utungaji na utekelezaji wa mipango na sera za kiuchumi.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 29, 2021 Ikulu jijini Zanzibar mara baada ya kupokea taarifa ya utafiti huo ambao utasaidia katika kutafuta njia bora na zenye ufanisi katika kuuinua uchumi wa Zanzibar, taarifa ambayo ilitolewa na Taasisi ya “The Brent Hust Foundation”.
Akitoa shukurani zake kwa timu hiyo ya utafiti, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, kuna kila sababu ya kuipongeza timu hiyo ambayo imefanya utafiti huo tena kwa kipindi kifupi ikiwa na lengo la kufanikisha njia bora za kuuinua uchumi wa Zanzibar.

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imejikita zaidi katika sera yake kubwa ya uchumi wa Buluu kutokana na Zanzibar kubarikiwa na rasilimali nyingi za bahari.

Amesisitiza kwamba, hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kutambua kuwa licha ya Zanzibar kuzungukwa na bahari, lakini inaonekana kwamba bado bahari haijatumiwa ipasavyo katika suala zima la uchumi.
Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha Sera hiyo ya Uchumi wa Buluu inaimarika kuna sekta muhimu ambavyo zimepewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii, uvuvi,miundombinu pamoja na sekta ya mafuta na gesi asilia.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, licha ya changamoto zilizokuwepo ikiwemo ya mtaji, lakini bado juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kwamba anafarajika kwa kuna wapo wanaojitokeza kuunga mkono juhudi hizo.

Rais Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Olusegun Obasanjo na timu yake akiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya “The Brent Hust Foundation” Greg Mills pamoja na Jonathan Oppenheimer ambaye ni Mwanzilishi wa taasisi hiyo ambao wamekuja Zanzibar kushiriki katika utoaji wa taarifa hiyo pamoja na kushirikiana nao katika uzinduzi wa kitabu cha cha “Asian Aspiration Book” cha Rais Olusegun Obasanjo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia kwamba Serikali yake itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kupitia utafiti huo pamoja na rai mbalimbali zilizotolewa katika utafiti.

Pia, Rais Dkt. Mwinyi amesema, kwamba amefurahishwa kuona kwamba mambo mengi yaliyobainika katika utafiti huo yameonekana kuwa yanakwenda sambamba na mikakakti iliyopangwa kutekelezwa na Serikali jambo ambalo alisema litasaidia sana katika kufikia malengo yaliyowekwa.

Amesema, kwamba ni kweli maendeleo yanayohitaji mitaji na rasilimali watu, hata hivyo kazi kubwa inahitajika na taasisi hiyo katika utafutaji wa mitaji ambayo ndiyo kikwazo kikubwa hivi sasa.

Kuhusu rasilimali watu, Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba, Zanzibar ina wafanyakazi wengi waliosomea fani mbalimbali ambapo hata hivyo aliahidi kushirikiana na taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo.
Mapema akitoa maelezo yake Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo amesema kuwa, ana matumaini makubwa kwamba uchumi wa Zanzibar utaimarika hiyo ni kutokana na mikakati maalum iliyokwekwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi.

Katika maelezo yake amesema kuwa, utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya “The Brent Hust Foundation”, utakuwa chachu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuyafikia malengo iliyojiwekea.
Nae Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alieleza imani yake juu ya utafiti huo uliofanywa hapa Zanzibar ambao utaleta majibu chanya katika kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio kama ilivyopata visiwa vingine vikubwa ambavyo vimezungukwa na bahari.

Akitoa taarifa ya utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa utafiti huo, Ray Hartley alieleza jinsi utafiti huo ulivyofanywa na hatimaye kuweza kupata mafanikio makubwa.

Amesema kwamba, ili Zanzibar iweze kupata maendeleo zaidi ni vyema Serikali ikaweza kuchukua maamuzi magumu katika kutekeleza mambo yenye maslahi mapana kwa taifa na wananchi kwa ujumla kwa kila pale inapobidi kufanya hivyo.

Vile vile, mtafiti huyo alihimiza umuhimu wa kukubali mabadiliko yanayotokezea baadhi ya wakati katika utendaji.
Ray Hartley alitumia fursa hiyo kueleza jinsi ya sekta mbalimbali ambazo iwapo zitafanyiwa kazi ipasavyo zitasaidia kukuza na kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwemo sekta ya utalii, uvuvi, kilimo na nyinginezo.

Pia, alitumia fursa hiyo kueleza jinsi maradhi ya COVID 19 yalivyopelekea kudhorotesha kuimarika kwa uchumi wa dunia ikiwemo Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments