Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa taasisi zinazowasafirisha Mahujaji, Masheikh na Walimu kwenda Hijja

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazowasafirisha Mahujaji pamoja na Masheikh na Walimu kuendelea kuwapa moyo Waislamu waliokosa fursa ya kwenda Hijja kutokata tamaa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba katika hotuba yake ya Baraza la Idd el Hajj aliyoitoa kwa wananchi.

Katika maelezo yake, Alhaj Dkt. Miwnyi alieleza kwamba kwa wale ambao walifikia hatua ya kutoa gharama za safari waondolewe shaka kuwa fedha zao ziko salama hadi Mwenyezi Mungu atakapowezesha kwenda kutimiza wajibu huo kama walivyoazimia.

Hivyo, aliwataka waumini kufuata mafundisho ya Uislamu ku katika hali kama hiyo waendelee kuwa na subira, wasichoke kuomba dua na kubaki katika Imani na uchamungu.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Saudia Arabia lilitangaza kuwazuwia Waislamu kutoka nchi za kigeni kwenda kuitekeleza ibada ya Hijja kwa mwaka huu kutokana na kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa COVID 19 katika Mataifa mbali mbali duniani.

Alisema kuwa, hali hiyo kwa mara nyengine imesababisha Waislamu wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa mwaka wa pili mfululizo wamekosa fursa ya kwenda Hijja licha ya maandalizi ambayo walikuwa wameshayaanza.

Kwa upande wa chanjo ya COVID 19 kwa Mahujaji kama sharti ilivyowekwa na Serikali ya Saud Arabia, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ilikuwa iko katika hatua za mwisho za kuwapatia chanjo wananchi wote waliodhamiria kwenda kuitekeleza ibaada ya Hijja kama ni sharti lililowekwa na Seriiali ya nchi hiyo.

“Tulipokee tukio hili kuwa ni miongoni mwa mitihani ambayo Mwenyezi Mungu ametuahidi katika Kitabu chake Kitukufu cha Qurani kwamba atatutahini kwa namna mbalimbali,”alisema Alhaj Dkt. Mwinyi.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi alitoa shukurani za dhati kwa viongozi na wananchi wote wa Pemba na hasa wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mapokezi yao pamoja na ushirikiano wao ambao umechangia kufanikisha shughuli hiyo iliyofana sana.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbali mbali kwa ajili ya kufanikisha dhamira ya kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalum la kimkakati la uwekezaji.


Alifahamisha kwamba, Serikali inaendeleza mazungumzo na wawekezaji walioonesha dhamira ya kushirikiana nasi katika suala hili, hasa katika kukiimarisha Kiwanja cha ndege cha Pemba, ujenzi wa bandari na miundombinu ya barabara.

“Tuendelee kuwa na subira na kushirikiana na Serikali ili kuweza kutimiza azma yetu hiyo,”alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Alisisitiza kwamba utii wa sheria una mchango muhimu katika kuendeleza amani na utulivu tulio nao nchini.

Aliongeza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha neema hizo zinawafikia wananchi wote hivyo alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi za kijamii, wazazi, walezi na wananchi, wote kuendelea kuhimizana katika kuidumisha na kuiendeleza amani iliyopo kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Katika kufikia dhamira ya kudumisha amani, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwahimiza wananchi wote kuungana katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na watoto pamoja na biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kuwa, Serikali imefungua ukurasa mpya katika kukabiliana na vitendo viovu ambavyo vinachangia sana kuhatarisha amani nchini ambapo hatua mbali mbali za kushughulikia kesi za udhalilishaji zinachukuliwa ili kuongeza kasi na namna bora zaidi ya kukabiliana na vitendo hivi vinavyoidhalilisha jamii, kuharibu taswira ya nchi na mustakabali wa vijana.

Aliongeza kuwa akiwa mzazi, anawasihi wazazi wenzake na walezi kushirikiana katika malezi ya vijana ili wawe na maadili mema yatakayowasaidia na kuwalinda na kujiingiza katika vitendo viovu.

“Tuwaase watoto wetu wajiepushe na marafiki wabaya, waongeze bidii na waweke mazingatio zaidi katika masomo yao ili tupate raia wema, wazalendo,wenye taalumu na maadili mema,”alisisistiza Alhaj Dkt. Mwinyi.

Viongozi kadhaa walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Mawaziri, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Al Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, wake wa viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wanawake pamoja na wananchi mbalimbali.

Mapema asubuhi, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada tukufu ya swala ya Eid-el Hajj iliyoswaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.Waislamu mbali mbali wamehudhuria katika viwanja hivyo na kuungana pamoja na Rais Dk. Mwinyi katika kutekeleza Ibada ya Swala ya Eid ya kuchinja ambayo huswaliwa baada ya waumini kutekeleza ibada tukufu ya Hijja huko Makka.


Akitoa hotuba ya Sala ya Idd El Hajj Sheikh Abdulrahman Bin Hilal alisema, kuwa lengo la kuwepo kwa Ibada ya Hijja ni kithibitisho cha imani ya mja na kuwa karibu na Mola wake.Mara baada ya kumaliza kusali sala hiyo ya Idd El Hajj, Alhaj Dk. Mwinyi alitekeleza sunna ya kuchinja tukio alilolifanya huko katika viwanja vya nyumba ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba.


Baada ya hapo, Alhaj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kukutana na kusalimiana na Masheikh pamoja na viongozi wa Dini wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba ambao walimuombea dua pamoja na kuiombea nchi na wananchi wote.Katika hafla hiyo Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Waumini wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba kwa kujitokeza kwa wingi katika Sala ya Idd el Hajj na kueleza jinsi alivyofarajika na umati mkubwa wa Waumini hao waliohudhuria katika sala hiyo huku akitumia fursa hiyo kusisitiza amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news