Rais Samia apokea Ripoti Maalum kuhusu BoT, taarifa ya maandalizi ya Sensa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya Ukaguzi Maalum kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayohusu matumizi ya fedha zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kati ya Januari na Machi mwaka huu.

Taarifa hiyo inatokana na agizo alilolitoa Rais Samia Machi 28, 2021, wakati akipokea Taarifa ya CAG kwa mwaka 2019/ 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea Taarifa ya Ukaguzi Maalum inayohusu matumizi ya Fedha zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kati ya mwezi Januari na March mwaka huu, kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere Jijini Dodoma leo Julai 01,2021.(Picha na Ikulu).

Rais Samia amepokea ripoti hiyo leo Julai 1, 2021 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo katika taarifa ya ukaguzi maalum, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, amesema katika ukaguzi uliofanyika imebainika kuwa fedha zilizotolewa BoT katika kipindi hicho zilifuata taratibu zote, isipokuwa baadhi ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika taasisi mbalimbali za Serikali yalibainika kuwa na mapungufu.

Mapungufu hayo ni pamoja na baadhi ya taasisi kama vile Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika.

CAG Kichere amesema, yamejitokeza mapungufu ambapo baadhi ya Makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo yao hali inayosababisha madeni ya makandarasi kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali.

Mapungufu mengine ni pamoja na kuwepo kwa miradi ambayo haikupangwa na hivyo kufanya malipo nje ya bajeti ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amepokea taarifa ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, 2022 kutoka kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea Taarifa ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi, inayotarajiwa kufanyika mwezi Agost,2022, kutoka kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa, leo Julai 01,2021 Jijini Dodoma.(Picha na Ikulu).

Dkt. Chuwa amesema, Sensa ya mwaka 2022 itatumia teknolojia ya kisasa ya Kidijitali chini ya mfumo ulipo wa Serikali katika ngazi zote za Utawala kwa pande zote za Muungano.

Aidha, amesema Sensa ya majaribio itafanyika mwezi Agosti mwaka huu (2021) katika mikoa saba kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments