Rais Samia ateta na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya kupitia mtandao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amezungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya Mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel, leo Julai 12,2021 Ikulu Jijini Dodoma. (Picha na Ikulu).

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Julai 12, 2021 Ikulu jijini Dodoma ambapo viongozi hao wawili walizungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na umoja huo.

Michel amempongeza Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua tangu kushika hatamu ya uongozi na kumhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

Aidha,Michel amempongeza pia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona. Vilevile alimueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

Kwa upande wake Rais Samia ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii na kuwekeza katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya EU.

Rais Samia amesema kuwa, benki hiyo imetoa Euro milioni 50 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege vya mikoani.

Amesema, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hususani matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Rais Samia amesema, kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Aidha,Rais Samia amemhakikishia Michel kuwa utawala wake utasimamia na kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za msingi za binadamu.

Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Rais Samia amemtaarifu Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Michel kuwa Tanzania tayari imeshajiunga na Mpango wa Kimataifa wa ugawaji wa chanjo kwa nchi masikini (COVAX) na ina Mpango wake wa taifa wa kupambana na Corona unaoainisha mahitaji ya nchi hivyo itawasilisha mahitaji yake kwa EU ili kupata msaada.

Rais ameshukuru kupokea mualiko wa kutembelea Umoja wa Ulaya na kumtumia salamu Rais wa Umoja huo, Ursula von der Leyen.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news