Rais Samia atoa pole kwa wafanyabiashara Kariakoo, Shule ya AT TOWN

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na kuungua moto kwa Soko Kuu la Kariakoo lililopo jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Samia ameyasema hayo leo Julai 11, 2021 ambapo kufuatia hasara kubwa iliyotokana na kuungua kwa soko hilo usiku wa Julai 10, 2021 ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto huo.

Amesema, Soko kuu la Kariakoo ni soko kubwa jijini Dar es salaam ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara na kuteketea kwa soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa wapangaji na wamiliki wa soko hilo kongwe nchini.

Rais Samia amesema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi, lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara kwa wafanyabiashara tu bali hata kwa Serikali.

Wakati huo huo,Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella na Jumuiya za Kiislaam Tanzania kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana AT TOWN inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislam iliyopo mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.

Rais Samia alisema, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuungua moto kwa shule zinazomilikiwa na jumuiya za dini nchini hivyo ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na jumuiya hizo kutafuta vyanzo vya matukio hayo na kuyadhibiti ili matukio ya kuungua moto kwa shule hizo yasijirudie.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news