RC ataka kilimo kidigitali kwa wakulima wa Mbeya

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imetoa changamoto kwa Kampuni ya Mbolea ya Yara, kuhakikisha programu mpya ya yaraConnect inayotoa elimu ya utaalamu wa kilimo kwa njia ya kidigitali waliyoizindua mkoani humo ikiwalenga wauzaji wa pembejeo za kilimo za Yara inawezeshwa ili iwe rahisi kutumiwa pia na wakulima ambao ndio walengwa wakuu wa mbolea ya Yara.

Changamoto hiyo imetolewa mkoani humo leo na mkuu wa mkoa huo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji wa Mbeya, Said Maditto akisema endapo wakulima wakiwezeshwa kutumia programu hiyo itawasaidia kupata elimu moja kwa moja kutoka Yara kuhusu matumizi ya mbolea wanayonunua kutoka kwa wauzaji jambo litakalosaidia kuwapa ufanisi wa haraka.

“Wakulima wakiwezeshwa kuwasiliana moja kwa moja Yara itasaidia kutoa changamoto zao moja kwa moja Yara kuhusu ufanisi ama tatizo lolote walilolipata kutoka kwenye bidhaa waliyonunua kutoka kwa wauzaji hivyo kuwawezesha Yara kutoa ufumbuzi wa changamoto zao,”amesema.

Pamoja na hayo aliishukuru Kampuni ya Yara kwa mradi wa kutoa msaada wa mbolea ili kusaidia matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la Covid-19 kwa mwaka jana ulipewa jina la ‘Action Africa’ ambapo Mkoa wa Mbeya pekee ulipewa tani 1,683 kati ya tani 13,951 zilizotolewa msaada nchi nzima akisema msaada huo umeongeza kwa kiasi kikubwa imani ya wakulima wa Mbeya kwa bidhaa za Yara.

“Ni matumaini yetu sisi kama serikali wakulima wa Mbeya wataendelea kutumia bidhaa za Yara na kama ilivyoelezwa kupitia programu hii italeta manufaa kwa wauzaji kwa upande mmoja na wakulima upande mwingine, hivyo ni matumaini yetu kuwa wadau wote wataitumia App hii vizuri kwa malengo ya kupata ufanisi na maendeleo zaidi katika kilimo chetu hapa Mbeya,”amesema.

Naye Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Mtei amesema, programu hiyo waliyoizindua itawasaidia wafanyabiashara hao kuaminika kwa wateja wao kwani mkulima huwa na desturi ya kuwa na imani na utulivu aendapo kwa muuzaji ambako maswali yake yatajibiwa kwa usahihi.

“Ninyi ni mabalozi wetu, na mpo karibu zaidi na walengwa wa bidhaa zetu ndio maana kupitia App hii tumeanzisha mpango wa uaminifu wa malipo kwa wafanyabiashara rejareja ili kuwapa pointi kwa mauzo myafanyayo kupata zawadi mbalimbali kuanzia simu za mkononi, pikipiki na fedha taslimu,”amesema.

Akijibu baadhi ya maswali kuhusu ubora wa mbolea ya Yara Bwana shamba Mwandamizi wa Yara, Maulidi Mkima amesema ili kupata matokeo bora ni vyema wakulima wakaelekezwa kufuata kanuni zote za matumizi ikiwemo vipimo sahihi na wakati sahihi wa matumizi ili kuepuka matokea yasiyorisha.

Naye mmoja wa wauza mbolea wa Mbeya, Daudi Nyassa ametoa wito kwa serikali na mamlaka husika kuangalia tatizo la kupanda kwa bei ya mbolea kila mara na pia kushuka kwa bei ya mazao kipindi cha mavuno jambo linaloleta athari kwa wakulima na kwa wauza pembejeo za kilimo.

“Mkulima anaponunua pembejeo kwa bei za juu kisha akauza mazao yake kwa bei ya chini hataweza kurudisha gharama za uzalishaji hivyo kufanya kilimo kisichokuwa na tija jambo ambalo litaweza kuleta athari katika mnyororo wote wa thamani wa kilimo chini,”amesema bwana Nyassa.

Huu ni mkoa wa sita sasa kwa Kampuni ya Yara kuzindua programu ya yaraConnect, jumla ikipanga kuzindua mikoa saba ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro.
Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji wa Mbeya, Said Maditto akizungumza na wauza pembejeo za kilimo wa Mkoa wa Mbeya na Songwe na wadau wengine wa mbolea ya Yara wakati wa uzinduzi wa programu ya yaraConnect mjini Mbeya. Alimwakilisha mkuu wa mkoa huo katika uzinduzi huo. Kushoto kwake ni Bwanashamba Mwandamizi wa Yara, Mauidi Mkima, Meneja Biashara Kanda ya Kusini, Andrew Ndundulu na Meneja Masuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Mtei.

Post a Comment

0 Comments