RC Dkt.Sengati aitaka jamii kuacha unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu

Na Anthony Ishengoma, Shinyanga

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Philemon Sengati amesema bado kuna changamoto ya unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu katika jamii kwani bado kuna baadhi ya wazazi na walezi ambao bado wanaficha ndani watu wenye ulemavu na kuwakosesha haki na huduma muhimu pamoja na Serikali kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu elimu kwa watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akiongea na Kamati ya Ushauri ya Watu wenye Ulemavu Mkoa Shinyanga wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo.Dkt. Sengati ametoa rai kwa familia zenye watu walemavu kutowaficha ndani na kuwataka kutambua kufanya hivyo ni kuwanyima fursa ya kupata elimu ambayo ni yao ya msingi kama ilivyo kwa watu wengine katika jamii.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga na kuzitaka halmashauri kote mkoani Shinyanga kuendelea kushirikiana na kamati za walemavu ikiwemo kutenga fedha asilimia mbili za mapato yao kwa ajili ya kutoa mikopo kuwezesha vikundi vya watu wenye mahitaji maalum.

Dkt.Sengati ameongeza kuwa, watu wanaoficha watu hao ndani wakibainika itabidi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kuhaidi kufanyia kazi changamoto zote wanazokabilianazo watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile akiongea na Kamati ya Ushauri ya Watu wenye Ulemavu Mkoa Shinyanga wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo.Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko ameitaka kamati hiyo pamoja na makundi mengine ya kijamii kuendelea kuhamasisha jamii kuacha tabia ya baadhi ya watu kuficha watu wenye ulemavu ndani ili waweze kupata fursa ya elimu kwani Mkoa wa Shinyanga una shule maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

‘’Tuendelee kuhamasisha ili wenyewe wasipate maangaiko, wasitumike vibaya waendelee kuwa kama watoto wengine na sisi serikali tutaendelea kuwahudumia kama tunavyotoa huduma na fursa kwa watoto wengine,"amesisitiza Jasinta Mboneko Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Watu wenye Ulemavu Mkoa Shinyanga wakifuatilia jambo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati hiyo.

Wakati huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga, Richard Mpongo akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa Mkoa aliwataka maafisa maendeleo ya jamii nchini kuendelea kuhamasisha watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo ya halmashauri kwa inayotolewa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mzee Mpongo aliongeza kuwa, pamoja na uwepo wa mikopo hiyo katika halmashauri vikundi vingi vya watu wenye ulemavu vimekuwa haviombi mikopo hiyo kutoka na makundi hayo maalum katika jamii kukosa elimu ya uwepo wa fursa hiyo hivyo kushindwa kuitumia kama ilivyopendekezwa na serikali.

Kamati hiyo ya Ushauri ya Mkoa wa Shinyanga inakaa kwa siku moja Manispaa ya Shinyanga kujadili masuala mbalimbali yahusuyo makundi mbalimbali ya jamii ya watu wenye ulemavu ili watoe mapendekezo yao kwa Mkoa kwa ajili ya utekelezaji na ushauri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news