SERIKALI KUIFANYIA MAREKEBISHO SHERIA YA VYAMA VYA USHIRIKA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali inafanya marekebisho ya sheria ya vyama vya ushirika nchini ili kuhakikisha kuwa mali na shughuli zote za vyama hivyo zinasimamiwa na wanachama wenyewe.

Lengo la marekebisho ya sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2013, ni kuhakikisha kwamba vyama vya ushirika vinajisimamia vyenyewe bila kuingiliwa na viongozi kutoka serikalini.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alibainisha hayo wakati wa siku ya maadhimisho ya siku ya ushirika duniani iliyofanyika kitaifa mwishoni mwa wiki mkoani Tabora.

Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu ‘Ushirika Pamoja, Tujenge Upya kwa Ubora na Tija’ alikuwa Waziri Mkuukuu, Kassim Majaliwa.

“Ushirika haulazimishwi kwa kuwa si mali ya serikali na kujiunga ni hiari hakuna mtu anayelazimishwa, mamlaka ya serikali katika ushirika yana mipaka yake,’’ alisisitiza.

Prof Mkenda aliongeza kuwa  hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kuviagiza vyama vya ushirika kutoa fedha katika akaunti zao kwa ajili ya matumizi yoyote.

“Ushirika ni hiari na mali ya wanaushirika, hivyo wanachama wanatakiwa kujua kwamba ni mali yao, wasimame kidete kusimamia shughuli zao bila kuingiliwa kinyume na utaratibu na sisi viongozi wa serikali lazima tujue mipaka yetu,’’ alisema na kuongeza:

“Hakuna ruhusa kwa kiongozi yeyote kwenda kuwapangia matumizi ya fedha zao.’’

Hata hivyo Waziri Mkenda alisema kuwa serikali ina wajibu kwenye ushirika kwa sababu wanaushirika ni wengi na kuna viongozi wao na pia kuna sheria inayowatambua.

“Ndani ya serikali kazi yetu ni kuhakikisha sheria inafuatwa, viongozi wanawajibika kwa wanaushirika wao na maamuzi yote ya wanaushirika yanafanywa na wanachama na si kukundi tu cha watu wachache,’’ alisema.

Prof Mkenda aliongeza kuwa serikali itaendelea kusimamia ushirika kuhakikisha kuwa unasimamiwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili kuhakikisha kuwa watu wengi wanapenda na kukubali kujiunga na vikundi mbalimbali vya ushirika.

Kila mwaka, siku ya ushirika duniani huadhimishwa kila siku ya jumamosi ya kwanza ya mwezi wa saba. Kwa mara ya kwanza siku hii iliadhimishwa chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa mwaka 2005.

Madhumuni ya maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa wanaushirika na kuimarisha mafanikio ya umoja wa kimataifa, uchumi endelevu, usawa na amani kote duniani.

Siku hii pia ina lengo la kuendeleza na kutanua ushirikiano baina ya ushirika wa kimataifa na nchi zingine duniani ikiwemo kushirikisha serikali kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news