Serikali kukarabati Barabara ya Manyata-Usa River kumuenzi Dkt.Anna Mghwira

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Ally Mwalimu, ameagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) kuikarabati barabara ya Manyata Usa-River ikiwa ni sehemu ya kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mstaafu, Marehemu Anna Mghwira.
 Mhe. Ummy ametoa agizo hilo leo Julai 26, 2021 alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibada ya mazishi iliyofanyika Usa-River, Halmashauri ya Meru, Wilayani Arumeru.

Pia, Waziri Ummy amesema Mheshimiwa Rais ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa kwa kuondokewa na Mama Mghwira ambaye alikuwa kiongozi jasiri, mwalimu na mshauri mwenye maono makubwa.

Waziri Ummy ametoa wito kwa wanawake wote kufuata nyayo za Mama Anna Mghwira kwa kuchapa kazi kwa bidii.

Mama Anna Mghwira alifariki dunia Julai 22, 2021 katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Marehemu Anna Mghwira amehifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele leo tarehe 26 Julai, 2021 Makumira Wilayani Arumeru ambapo mazishi yake yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikari wakiwemo Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watumishi wa Serikali wa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Post a Comment

0 Comments