Serikali: Ujenzi wa Reli ya SGR kutoka Mwanza hadi Isaka kuwanufaisha wananchi

Na Hellen Mtereko, Diramakini Blog

Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka wenye urefu wa kilomita 341 unatarajiwa kuwanufaisha wananchi kwa kutoa ajira 11,000.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (katikati), Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya uelewa wa mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tano Mwanza hadi Isaka.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kampeni ya uelewa kwa jamii juu ya mradi wa ujenzi huo.

Amesema, ujenzi huo ni kipande cha tano awamu ya kwanza ambao kwa hapa Mwanza utahusisha maeneo ya Nyamagana, Kwimba na Misungwi.

Amesema kuwa,pamoja na ajira hizo kutolewa pia wafanyabiashara wakubwa wajiandae kwa ajili ya kujenga maghala na kuwa na kituo cha biashara.

Amesema, kwa wale wananchi ambao mradi huo utapita katika maeneo yao watalipwa fidia kulingana na Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999.

"Nawahakikishia wananchi hakuna ambaye hatapata haki yake,hivyo kwa wale wote watakaopitiwa na mradi huo lazima wapate sitahiki zao,"amesema Luhumbi.

Kwa upande wake Meneja mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR Mwanza hadi Isaka, Machibya Masanja amesema, kampeni hiyo ilianza 28 Juni,2021 kwa lengo la kuhakikisha elimu inawafikia Watanzania na kunufaisha Taifa katika kuimarisha mahusiano kati ya mradi na wananchi wakati wa utekelezaji ili kufikia lengo la uendelezaji na ujenzi wa miundombinu ya reli nchini.

Amesema, kupitia elimu inayotolewa,wananchi watapata uelewa juu ya Ujenzi wa Reli,Elimu ya fidia na utwaaji ardhi,mazingira pamoja na ulinzi na usalama wa Reli.

Masanja amesema kuwa, kampeni hiyo ni endelevu na ni hatua muhimu ya awali katika utekelezaji wa mradi ili kutoa fursa kwa Wananchi kushiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Mitaa na vijiji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news