Serikali yatoa siku saba uchunguzi chanzo cha moto Soko Kuu Kariakoo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa ameipa siku saba za awali tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto katika Soko la Kimataifa la Kariakoo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo.

Ametoa kauli hiyo leo Julai 11, 2021 alipokuwa anazungumza na wafanyabiashara na wakazi wa eneo la Kariakoo baada ya kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa kudhibiti moto huo jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amesema kuwa, kamati iliyoundwa ambayo itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa huo itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo itawakilishwa na Mkurugenzi wa Maafa.

Wengine ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikujumuisha Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Zimamoto pamoja na Taasisi ya Kupambana na Rushwa. Pia Waziri Mkuu alizitaja Wakala wa Majengo, Shirika la Umeme (TANESCO), Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

“Endapo itagundulika kama kuna mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike moto,”amesema.

Aidha, Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara katika soko hilo wawe watulivu wakati Serikali inafanya kazi yake ya kujua chanzo cha moto huo na aliwahakikishia usalama wa mali zilizo ndani ya soko hilo.

Waziri Mkuu pia amewataka wafanyabiashara kutoingia ndani ya soko hilo katika kipindi hiki ambacho udhibiti unaendelea hadi pale timu zilizoundwa zitakapojiridhisha na utulivu na kufanya sensa ya watu wenye mali kuingia mmoja baada ya mwingine ili wakatoe vitu walivyoviacha.

“Tunachoshukuru kule chini shimoni hakuna moto, mali zote zinalindwa, msiwe na mashaka milango yote imefungwa na makamanda wako ndani na nje wanalinda, mali zote zimehifadhiwa, msiwe na mashaka,”amesema.

Kadhalika Waziri Mkuu aliwaahidi wafanyabiashara hao kuwa Serikali itaongea na mabenki yaliyowakopesha wafanyabiashara waliounguliwa na mali zao kuwaongezea muda wa kulipa mikopo yao baada ya kuunguliwa.

“Tume itapata taarifa za kila mmoja mwenye mkopo rasmi kwenye taasisi za fedha ili tuzungumze nao waongeze muda waache kipindi hiki ili uweze kulipa hapo baadae utakapo kuwa umetulia,biashara imeungua naamini mabenki yatatuelewa na kuweka utaratibu mzuri,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news