TCU yafungua dirisha la kwanza la udahili mwaka wa masomo 2021/2022

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua rasmi dirisha la kwanza la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (shahada ya kwanza) kwa mwaka wa masomo wa 2021/ 2022 huku ikianisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa ameyasema hayo leo Julai 12, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam.

Amesema, kufunguliwa kwa dirisha hilo kumekuja baada kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita Julai 10,2021.

Profesa Kihampa amesema, tume imefungua dirisha hilo jana badala ya Julai 15,2021 tarehe iliyokuwa imepangwa awali ambapo litakuwa wazi hadi Agosti 5,2021.

"Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU,tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada za kwanza pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari,"amesema.

Amesema,udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu kidato cha sita; wenye Stashahada (Ordinary Diploma); na waliomaliza programu ya ‘Foundation’ ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Prof.Kihampa amesema, ili kufahamu sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu waombaji wameelekezwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU huku pia wakitakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua na kwamba maelekezo ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo vikuu husika.

"Tunawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, kwani masuala muhimu ambayo waombaji wanapaswa kuzingatia ni pamoja na kusoma muongozo wa udahili na kuuelewa, kuingia kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektroniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news