Uhaba wa elimu matumizi ya mbolea watajwa kikwazo kwa wafanyabiashara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

IMEELEZWA kuwa uhaba wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo ni moja ya vikwazo vinavyowakabili wauzaji wengi wa pembejeo za kilimo hizo nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu mpya ya yaraConnect mkoani Njombe, Bwanashamba Mwandamizi wa Kampuni ya kusambaza Mbolea ya Yara Tanzania, Maulidi Mkima alisema, wauzaji wengi hawana elimu ya bidhaa wanazoziuza matokeo yake ni kutoa mrejesho usio sahihi kwa wakulima hivyo kuwafanya wakulima na watumiaji wengine wa pembejea hizo kutopata matokeo yenye tija.

“Mathalani kuna tofauti kati ya mbolea moja na nyingine katika matumizi yake, hivyo endapo wauzaji watapata elimu ya kutosha itawasaidia, ni vyema wauzaji paia wakatumia vyema programu ya yaraConnect ili kujipatia elimu mbalimbali ya matumizi bora ya mbolea na pembejeo nyingine ili kumuwezesha mkulima kufanya kilimo chenye tija,"amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo, Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Njombe, Wilson Joel amesema, kwa kupitia mfumo wa programu ya yaraConnect ni imani yao kama serikali pamoja na wadau wa kilimo itawasaidia kufikia malengo waliyojiwekea katika kufanya kilimo chenye manufaa mkoani humo.

Meneja Msuluhisho ya Kidigitali wa Yara, Deodath Matei alisema programu hiyo inayowalenga wauzaji wa bidhaa za Yara ina faida mbili, moja ikiwa kupata elimu ya kilimo ambayo wao wanaulizwa mara kwa mara na wakulima pindi wanapokwenda kununua bidhaa kwao na pili kupata zaidi katika miamala wanayofanya wakiuza bidhaa za Yara.

“Watapata thamani zaidi kwa miamala yao wanayoifanya wanapouza bidhaa Yara itawaongezea pointi na watazitumia ili kupata zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslimu, simu za mikononi na pikipiki, kuwa na app hii ni sawa na kuwa na bwanashamba mkononi kwani maswali mengi ya wakulima yanajibiwa na mfanyabiashara anaweza kuuliza swali papo hapo na kupata majibu kutoka kwa wataalamu wa Yara,”amesema Mtei.

Naye mmoja wa wafanyabisahara wa mjini Njombe, Ester Simon ameishukuru kampuni ya Yara kwa kuwaletea programu hiyo kwani sasa anauhakika wa kuwa na majibu ya kila swali linaloulizwa na wakulima wanapokuja dukani kwake kununua bidhaa za Yara hivyo kujijengea uaminifu kwa wateja wake.

Meneja Huduma kwa Wateja Kidigitali wa Kampuni ya Mbolea ya Yara, Eva Sauwa (kulia) akitoa maelekezo kwa mmoja wa wauza pembejeo za kamupuni hiyo katika hafla ya uzinduzi wa programu ya yaraConect kwa Mkoa wa Njombe ambapo pamoja na mambo mengine wauzaji hao wa pembejeo za Yara walipewa mafunzo mbalimbali ya matumizi ya programu hiyo na masuala mengine ya kitaalamu kuhusu kilimo na jinsi watakavyoweza kuwasaidia wakulima ambao ndio wateja wao kitaalamu. Hafla hiyo ilifanyika mjini Njombe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news