Ujenzi Chuo cha VETA Mlola watoa fursa kwa wananchi Lushoto kuimarisha uchumi

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MRADI wa ujenzi wa Chuo cha VETA Mlola kilichopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga umetoa fursa kwa wananchi wa kata mbili za Mlola na Makanya kuweza kuuza kokoto, mawe na mchanga, huku wanawake wakiwa wanufaika wakubwa.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, Shaaban Shekilindi (kushoto) akikagua Chuo cha VETA kinachojengwa Kata ya Mlola wilayani Lushoto. Wengine ni Diwani wa Kata ya Makanya Zaniali Mohamed (katikati) na Ofisa Mipango Wilaya ya Lushoto Doroth Mungure (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi akiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake wanaoponda kokoto kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Lushoto kinachojengwa Kata ya Mlola. (Picha na Yusuph Mussa).

Mwandishi wa habari hii alifika Julai 16, 2021 eneo ambalo wanawake wanatumia fursa ya kuponda kokoto na kuuza kwa mkandarasi anaejenga chuo hicho ambaye ni Chuo cha VETA Moshi mkoani Kilimanjaro ambacho kinajengwa kwa Force Account (Wataalamu wa ndani).

Maimuna Ngereza alisema ujio wa chuo hicho ambacho kinajengwa katika Kijiji cha Mbula, Kata ya Mlola, kimewasaidia kupata ajira ya muda, kwani wanafanya kazi ya kuponda kokoto na kuuza huko, hivyo kuweza kupata pesa.

"Chuo hiki kwetu kimekuja kutukomboa kwa kupata ujira, kwani tunaponda kokoto na kwenda kuuza kwenye chuo hicho. Hivyo tunapata mahitaji ya nyumbani ikiwemo chakula, mavazi na pesa za matumizi mengine," alisema Ngereza.
Ujenzi Chuo cha VETA kinachojengwa Kata ya Mlola wilayani Lushoto ukiendelea. (Picha na Yusuph Mussa).

Mariam Kingazi alisema, ukiacha shughuli za kilimo, baada ya msimu kupita wanakuwa hawana shughuli nyingine ya kufanya. Lakini ujio wa chuo hicho umewawezesha kuwa na kazi za kufanya kwa mwaka mzima, kwani chuo hicho kitakuwa na manufaa sana kwao, hasa kwenye kupata kipato.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi (katikati) akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kijiji cha Mbula, Kata ya Mlola ambao walilalamika kuwa wakati mwingine malipo yao yanachelewa. Ni yale ya ajira za muda katika ujenzi wa Chuo cha VETA Lushoto kinachojengwa Kata ya Mlola. Kulia ni Diwani wa Kata ya Makanya Zaniali Mohamed na kushoto ni Msimamizi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Lushoto Mhandisi Erick Kiboko. (Picha na Yusuph Mussa).

Zalika Kihiyo alisema, manufaa ya chuo hicho ni mengi, kwani pamoja na kuponda kokoto, bado kitawasaidia watoto wao kusoma hapo kuanzia wanafunzi waliomaliza darasa la saba na kuendelea. Hivyo wanashukuru kwa Serikali na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi maarufu 'Bosnia' kwa kupeleka chuo hicho Tarafa ya Mlola.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mbula katika Kata ya Mlola na wale wa Kata ya Makanya, Shekilindi alisema chuo hicho kinafungua fursa ya kiuchumi kwenye Tarafa ya Mlola katika Jimbo la Lushoto, kwani kuwepo kwa chuo hicho, ukiacha shughuli za ujenzi wa chuo, pia kitasomesha watoto wao, watauza vyakula kwa wanachuo na wakufunzi, na wataweza kupangisha nyumba kwa wakufunzi na wanafunzi watakaoishi nje ya chuo.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi (wa pili kulia) akipewa maelezo na Mhandisi Erick Kiboko (katikati fulana ya bluu) juu ya maendeleo ya Chuo cha VETA kinachojengwa Kata ya Mlola wilayani Lushoto. (Picha na Yusuph Mussa).

"Chuo hiki kina fursa nyingi. Pamoja na kushiriki shughuli za ujenzi, lakini kitachukua hata wanafunzi waliomaliza darasa la saba na kuwapa ujuzi wa aina mbalimbali ili waweze kujiajiri na kuajiriwa kwenye nyanja mbalimbali. Lakini kwa kuwepo chuo hiki Mlola kutaongeza shughuli za kiuchumi kwa kuuza vyakula ikiwemo mahindi, maharage na mbogamboga.

"Ombi langu msiuze maeneo ya ujenzi wa nyumba kiholela, na mnapouza basi iwe kwa bei ya juu ili na ninyi mnufaike, na muwe na uhakika majirani mnaowauzia maeneo hayo ambao watajenga nyumba za makazi na biashara, wawe watu mnaowajua hawataweza kuwaletea shida baadae," alisema Shekilindi.
Mtendaji wa Kata ya Makanya wilayani Lushoto Johari Ndossy akieleza kuwa ni lazima wananchi wajenge vyoo. Alitoa ufafanuzi huo kwenye mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi. Ni baada ya wananchi wa Kijiji cha Mdando kulalamika kuwa nguvu kubwa zinatumika kwenye utekelezaji wa zoezi hilo. (Picha na Yusuph Mussa).

Shekilindi alisema chuo hicho ni mkombozi kwa wananchi wa Wilaya ya Lushoto, kwani pamoja na kwamba kitachukua wanafunzi kutoka pembe zote za nchi, lakini kipaumbele kitakuwa kwa vijana wa majimbo matatu ya wilaya hiyo ikiwemo Jimbo la Lushoto, Mlalo na Bumbuli, hivyo wazazi wajipange kusomesha watoto wao.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi akiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake wanaoponda kokoto kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Lushoto kinachojengwa Kata ya Mlola. (Picha na Yusuph Mussa).

Msimamizi wa ujenzi huo kutoa Chuo cha VETA Moshi Mhandisi Erick Kiboko alisema ujenzi wa Awamu ya Kwanza wa chuo hicho ulianza Februari 24, mwaka huu, na unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani. Mradi huo wa Awamu ya Kwanza unajengwa majengo 17 pamoja na samani zake kwa gharama ya sh. bilioni 1.6.

Mhandisi Kiboko alisema wananunua kokoto za wananchi kwa ajili ya kutandika jamvi (msingi wa jengo) kwa sh. 63,000 kwa ujazo wa kilo 1,000, huku mawe yenye ujazo wa kilo 1,000 wananunua kwa sh. 30,000 na mchanga wenye ujazo wa kilo 1,000 wananunua kwa sh. 20,000.

Post a Comment

0 Comments