Waliohitimu mafunzo SIDO watakiwa kuwa wabunifu

Na Derick Milton, Busega

Wito umetolewa kwa vijana waliohitimu mafunzo ya utengenezaji bidhaa za ngozi katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu yaliyokuwa chini ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuwa wabunifu na kujituma.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa wilaya hiyo, Gabriel Zackaria, wakati akifunga mafunzo hayo kwa vijana zaidi ya 100 walitoka kwenye Wilaya ya Busega na Bariadi mkoani humo.

Zackaria amewataka vijana hao kutumia fursa waliyopata ya mafunzo hayo kwenda katika maeneo yao na kuanza kutafuta mbinu mbalimbali na kuwa wabunifu katika kuhakikisha elimu hiyo inawasaidia kwenye maisha yao.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa, haitakuwa vyema vijana hao baada ya kupata mafunzo hayo na kwenda nyumbani kwao kukaa bila ya kazi kutokana na kukosa mtaji.

Amesema kuwa fursa ya elimu ambayo wamepata kutoka SIDO ni kubwa sana kuliko mtaji, kwani amewataka kutumia nguvu zao wenyewe walizonazo kuanza kutengeneza bidhaa walizofundishwa kidogo kidigo.

“ Elimu hii ni kubwa sana, ikiwa mtaweza kuitumia vyema kuwa wabunifu, kujituma hakika wale ambao waliyakimbia watasikitika, siyo lazima ukaanze vitu vingi, anzeni kidogo kwa mtaji huo ulionao,” amesema Zackaria.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka vijana hao kujiunga katika vikundi na kuanzisha mradi unaoweza kutokana na mafunzo ambayo wamepata kasha serikali kupitia halmashauri waweze kupatiwa mkopo.

“ Kupitia mafunzo haya, nendeni mkajiunge katika vikundi, kuna fursa za mikopo kwenye halmashauri yetu ya Busega, lakini lazima mkaonyeshe nini mnafanya, anzeni kutengenza viatu, shanga, kama ambavyo mmefundishwa na hapo mtaweza kupewa mkopo,” ameongeza Zackaria.

Awali akiongea kwenye hafla hiyo Meneja SIDO mkoa, Athanas Moshi amesema kuwa mafunzo hayo yalikuwa ya wiki nne, ambapo mbali na kujifunza kutengeneza viatu vya kawaida na vyenye urembo, vijana hao wamefundishwa ujaslimali.

Moshi amesema kuwa Mafunzo hayo ambayo yametolewa mkoa mzima, SIDO imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ujaslimali ili waweze kujiajiri.

Meneja hiyo amewataka vijana hao kwenda kuunda vikundi na kuanza kutengeneza bidhaa ambazo wamejifunza kupitia mafunzo hayo, huku akiwahaidi SIDO kuwashika mkono katika kuwaongezea mtaji.

“ SIDO mbali na kutoa mafunzo haya, lakini tunatoa mtaji kwa watu ambao wanaonyesha njia kuwa wanaweza kuanza kufanya kwa kutumia nguvu zao, wapo baadhi ambao wamefanya na tumewapa mtaji lakini hata vifaa,”amesema Moshi.

Juma Alex mmoja wa vijana walihitimu mafunzo hayo ameshukuru SIDO kwa mafunzo hayo ambayo yanaenda kubadilisha maisha yako kwani wamekuwa wajasliamali na wenye uwezo wa kutengeneza bidhaa za ngozi kwa kiwango kikubwa.

“ Wote hapa tulikuja hapa hatujui kitu chochote, lakini leo ni wataalamu na tunaweza kwenda uko nyumbani tukaanza kutengeneza hata viatu, tunaiomba serikali kutusaidia eneo la mtaji kwani wengi wao tunatatoka familia duni,” amesema Alex.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news