Wizara yapiga marufuku kampuni za simu zinazowarubuni wananchi ujenzi wa minara

Na Faraja Mpina, Dodoma

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watendaji wa makampuni ya simu wasio waaminifu pamoja na washirika wao kuwarubuni wananchi kuuza maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano bila wao kujua kuwa wanauza kwa ajili ya ujenzi huo.
 Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (katikati) akizungumza katika eneo la ujenzi wa mnara wa TTCL katika kijiji cha Chang’ombe kilichopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma wengine ni watendaji aliombatana nao na wananchi wa eneo hilo.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Dodoma katika Wilaya ya Kongwa Mhandisi Kundo amesema kuwa kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kurubuniwa kuuza maeneo yao lakini baada ya muda mfupi minara ya mawasiliano inajengwa katika maeneo hayo ambapo kodi ya ardhi ya eneo husika inaanza kulipwa kwa mmiliki mpya na mwananchi aliyeuza eneo lake kwa gharama ndogo hapati chochote

Ameongeza kuwa inafahamika kuwa kila mtu ana haki ya kisheria ya kumiliki eneo, kuuza na kupangisha eneo lake kwa kodi atakayoona inafaa lakini kinachofanyika katika baadhi ya maeneo ni wananchi kushawishiwa kuuza maeneo yao bila kujua kuwa ni eneo linalokuja kufanyiwa uwekezaji baada ya kufanyiwa utafiti na kuonekana linafaa kujengwa mnara wa mawasiliano.Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia) akipokea zawadi ya gunia la mahindi kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Njoge alipofika kukagua ubora, uwezo na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kongwa.

“Jukumu la Serikali ni kulinda maslahi ya wananchi hivyo naelekeza kila Mkurugenzi wa Halmashauri anapaswa kutambua umiliki wa eneo husika kabla ya kutoa kibali cha ujenzi wa mnara wowote ili kujiridhisha kama mmiliki wa eneo hilo anatambuliwa na Serikali ya kijiji husika,”amesema Mhandisi Kundo.

Kwa upande wa malipo ya kodi ya ardhi kwenye maeneo yanayoenda kujengwa minara Mhandisi Kundo ameelekeza mikataba yote kufanyika kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwasababu yeye ndiye mwenye wataalam wanaojua thamani na gharama za maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri husika.Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kushoto) alipotembelea Ofisi za Shirika la Posta Wilaya ya Kongwa na kukagua utoaji wa huduma za Shirika hilo wakati wa ziara yake ya kukagua ubora, uwezo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katiak Wilaya hiyo. Wa kwanza Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remedius Mwema Emmanuel.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Mwema Emmanuel amesema kuwa katika Wilaya ya Kongwa kumekuwa na malalamiko mengi na migogoro kutoka kwa wananchi kuhusu kurubuniwa kuuza maeneo yao na wakati mwingine wenyeviti wa vijiji wamekuwa wakitumika kuhamasisha wananchi.

Ameongeza kuwa katika kata ya Nghumbi kijiji cha Mbagirwa kuna mnara wa mawasiliano lakini mmiliki wa eneo husika hajulikani na Serikali ya kijiji haipati kodi yeyote kutoka katika mnara huo.

Aidha, katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Naibu Waziri huyo ameendelea kupokea na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazogusa Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupokea mahitaji ya wananchi ya kuboreshewa huduma ya mawasiliano ya simu na intaneti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news