Bei za mafuta kuongezeka kuanzia kesho

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA BIDHAA ZA MAFUTA YA PETROLI KUANZIA JUMATANO, TAREHE 1 SEPTEMBA 2021

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 1 Septemba 2021. Pamoja na kutambua bei hizo, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:-
(a) Bei za rejareja na jumla za mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 4 Agosti 2021. 

Kwa Septemba 2021, bei za rejareja za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kwa shilingi 84/Lita (sawa na asilimia 3.47), Shilingi 39/lita (sawa na asilimia 1.74) na Shilingi 18/lita (sawa na asilimia 0.83), mtawalia. 

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kwa shilingi 83.84/Lita (sawa na asilimia 3.65), Shilingi 39.05/lita (sawa na asilimia 1.84) na Shilingi 18.05/lita (sawa na asilimia 0.88), mtawalia.

(b) Kwa mwezi Septemba 2021, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa tarehe 4 Agosti 2021. 

Kwa mwezi Septemba 2021, bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa shilingi 53/lita (sawa na asilimia 2.13) na shilingi 14/lita (sawa na asilimia 0.59), mtawalia. Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa shilingi 52.81/lita (sawa na asilimia 2.24) na shilingi 13.60/lita (sawa na asilimia 0.62) mtawalia. 

Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye maghala ya mafuta yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka Dar es Salaam. 

Hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo imekokotolewa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

(c) Kwa Septemba 2021, bei za rejareja na jumla kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa tarehe 4 Agosti 2021. 

Kwa mwezi Septemba 2021, bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Shilingi 108/lita (sawa na asilimia 4.50) na Shilingi 49/lita (sawa na asilimia 2.15), mtawalia. Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Shilingi 108.10/lita (sawa na asilimia 4.74) na shilingi 48.73/lita (sawa na asilimia 2.27), mtawalia. 

Kutokana na kutokuwepo kwa mafuta ya taa kwenye maghala ya mafuta yaliyopo Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka Dar es Salaam. 

Hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo imekokotolewa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

d) Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta (BPS Premium).

(e) EWURA inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.

(f) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. 

EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

(g) Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 656 la tarehe 21 Agosti 2020.

(h) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. 

Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

(i) Wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na Wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia, risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news