CCM RUANGWA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UTEKELEZAJI WA ILANI

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAJUMBE wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ruangwa wamempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 pamoja na usimamizi mzuri wa Serikali.
Mkutano huo umefanyika leo Agosti 18, 2021 Wilayani Ruangwa na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri hiyo ambayo imeelezea kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya sita na kuahidi kuendelea kuiunga mkono.

Pia, mkutano huo umepokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika wilaya hiyo iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma ambapo Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza wakuu wa idara kwa utendaji mzuri na kuwataka waongeze ubunifu.

“Kila mkuu wa idara ni muhimu akatekeleza majukumu yake kwa kufuata muongozo uliopo katika kitabu cha Ilani. Tekelezeni majukumu yenu kwa kuitafsiri Ilani ya uchaguzi, muone ndani ya kitabu hicho kimeeleza nini kuhusu idara zenu na mtekeleze,"amesema.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye amezungumza kwa niaba ya wajumbe wenzake wa mkutano huo amewasihi wajumbe hao pamoja na Wana-Ruangwa wote wawakaribishe wawekezaji wa sekta binafsi ili kuchangia katika ukuaji wa shughuli za maendeleo.

“Sekta binafsi ndio zinaleta maendeleo kwa kutoa mchango mkubwa Serikalini, hivyo kama yoyote ana rafiki ambae anaweza akajenga hoteli au kiwanda unaweza kumleta na akapatiwa ardhi kwa ajili ya kufanya uwekezaji,"amesema.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wajumbe wa mkutano huo wawahamasishe wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (UVIKO 19) kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na kwenda kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Akiwasilisha taarifa ya utekeleza wa Ilani katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo shilingi bilioni 4.316 zitakazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya elimu zikiwemo nyumba za walimu 21, ofisi za swalimu 37, madarasa 145, vyoo matundu 312.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news