Manchester City wasababisha kilio kwa Arsenal kupitia 5G

NA GODFREY NNKO

Manchester City wameendeleza kichapo cha nguvu baada ya kuiharibia wikiendi Arsenal kwa magoli 5-0.

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya England leo Agosti 28,2021 katika Uwanja wa Etihad.
Manchester City huo ukiwa ushindi wa pili katika mechi tatu, kufuatia kuchapwa 1-0 na Tottenham Hotspur na kushinda 5-0 dhidi ya Norwich City.

Pengine kwa Arsenal hii ni safari mbaya kwao, kwani wapo katika orodha ya vikosi vitatu vya mwisho kwa mara ya kwanza tangu Agosti 1992, Je? Watashushwa kwenye EPL? Subira ina majibu. Tuendelee...

Arsenal ambao ni mabingwa mara tatu wa EPL kwa sasa chini ya kocha Mikel Arteta,wamepoteza mechi zote tatu za kwanza muhula huu. Wamefungwa jumla ya mabao tisa na hawana goli wala alama yoyote kwa sasa.

Machozi yao yanaweza kuwa kwa Ilkay Gundogan, Ferran Torres na Gabriel Jesus ambao walifunga mabao ya Man-City katika kipindi cha kwanza kilichoshuhudia kiungo mkabaji wa Arsenal, Granit Xhaka ambaye ni raia wa Uswisi akionyeshwa kadi nyekundu.

Ni kwa kosa la kumchezea visivyo Joao Cancelo katika mtanange huo mtamu.

Rodri Hernandez alifunga bao la nne la Man-City katika dakika ya 53 kabla ya Torres kuachia chombo hatari ambacho kilififisha matumaini ya wageni wao dakika sita kabla ya kipenga cha mwisho.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Man-City kusajili ushindi wa 5-0 katika EPL katika uwanja wao wa nyumbani wa Etihad.

Walifunga kampeni za msimu wa 2020-21 kwa kuitandika Everton 5-0 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Norwich City wiki iliyopita ikiwa ni wiki moja baada ya kutandikwa 1-0 na Tottenham Hotspur katika mechi ya kwanza muhula huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news