Manispaa ya Kinondoni yatoa neno kodi za mabango

Na Anneth Kagenda, Diramakini Blog

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imeomba kurudishiwa huduma ya ukusanyaji Kodi za Mabango kwa kile kilichodaiwa kuwa kukosa huduma ya kukusanya kodi hizo kumekuwa kukisababisha baadhi ya changamoto za wananchi kutotatuliwa kwa wakati.
Wito huo umetolewa mkoani Dar es Salaam na Naibu Meya Manispaa ya Kinondoni Kheri Nassor Missinga maarufu 'Obama' wakati akiongea na DIRAMAKINI Blog.

Amesema, awali manispaa hiyo ilipokuwa ikikusanya kodi za mabango hayo kabla ya kuhamishiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), fedha ilikuwa ikiingia katika Manispaa hiyo na kwamba kiwango cha mapato kilichokuwa kikiingia kilikuwa ni kikubwa ambacho kwa namna moja ama nyingine pia kilikuwa kikifanya uharakishwaji wa utatuzi wa changamoto nyingi za wananchi Manispaa ya Kinondoni.

"Siyo kwamba kwa sasa changamoto hizo hazitatuliwi hapana, ila kuwepo kwa ukusanyaji wa kodi hizo pia ulikuwa ukiongeza spidi zaidi, hivyo basi tunaomba turudishiwe ili tuendelee kukusanya kodi wenyewe kodi hizi za mabango,"alisema.

Aidha, alisema pia wakati manispaa hiyo ikikusanya kodi hizo ilikuwa ikipata fursa ya kutatua changamoto nyingi tofauti na hali ilivyo sasa japokuwa huduma zinatolewa kwa wananchi, lakini si kwa kasi kubwa kama ya awali ambapo manispaa hiyo ilikuwa ikikusanya wenyewe.

"Ninachoweza kusema hapa ni kwamba tukikusanya kodi za mabango wenyewe kuna changamoto nyingi za wananchi tulikuwa tunazitatua kwa wakati lakini pia mabango yalikuwa ni moja ya vyanzo vikubwa vya mapato,"alisema Obama na kuongeza;

"Hivyo kutokuwepo kwa vyanzo hivyo kuna adhari japo tunavyo vyanzo vingine, ombi letu sasa turudishiwe kwani kuwepo na huduma hii pia kumekuwa kukitusaidia makusanyo yanakngezeka zaidi,.

Kuhusu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi kuhusiana na kutakiwa kulipia huduma za dawa ambapo inadaiwa dawa hiyo humwagwa kwenye mazalia ya mbu pamoja na chooni, Naibu Obama alisema siyo kweli kwamba Manispaa inatoza wananchi fedha.
"Siyo kweli kwamba Manispaa inauza dawa za kuua mazalia ya mbu wala mazalia ya wadudu wa chooni, bali manispaa ina oda dawa hizo na baadaye inatoa huduma bure na hatumlipishi mwananchi yeyote maana yake ni kwamba dawa kama dawa tunazitoa bure," alisema Obama.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi na kuwataka kuwa na ushirikiano baina yao na viongozi wa Manispaa hiyo pamoja na watendaji ili wananchi hao waweze kuhudumiwa kwa ufanisi zaidi na kupata huduma iliyo bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news