Mwalimu Makuru aibua hoja nzito kuhusu maendeleo mikoa ya Kusini

Na Amos Lufungilo, Diramakini Blog

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inapaswa kuungwa mkono na makundi yote kwani imeonyesha dhamira njema ya kustawisha maendeleo katika kanda zote hapa nchini.
Amesema, ni jambo la kufurahisha kuona tayari kuna mikakati kabambe ambayo inatekelezwa na Serikali kuhakikisha mikoa ya Kusini inafunguka kiuchumi hususani mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

"Ni dhairi kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imepanga na kupania kuinua uchumi wa mikoa ya Kusini, ambao ulikuwa umezorota na kudorora kwa miaka mingi kutokana na wawekezaji wengi waliokuwa wamewekeza katika mikoa hiyo ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kuamua kuacha uwekezaji na kuondoka, hivyo kusababisha uchumi wa mikoa hiyo ya Kusini mwa Tanzania kudorora;

Mwalimu Makuru ameyasema hayo mjini Musoma wakati akizungumza kuhusiana na fursa mbalimbali zilizopo Ukanda wa Kusini na namna ambavyo zinapaswa kutumika kwa maslahi ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Amesema. jambo la kipekee ambalo amelibaini mapema chini ya Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais Samia ni kutekeleza miradi ya maendeleo shirikishi na jumuishi katika kanda mbalimbali nchini ili kuwezesha kufungua fursa na kuwafungulia wananchi milango ya kustawi kiuchumi.

Mwalimu Makuru amesema, baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani wawekezaji wengi wameweza kujitokeza na kuja kuwekeza nchini katika nyanja za kibiashara na viwanda, hivyo Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuweka na kuruhusu mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yatajali manufaa ya pande zote kati ya Serikali, wananchi na wawekezaji.

"Hatua hii ni muhimu sana, na sisi wananchi tunapaswa kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali bega kwa bega wakiwemo wawekezaji ambao wameonyesha dhamira ya kuja kuwekeza katika maeneo yetu ili kupitia uwekezaji wao uweze kutupa fursa za ajira na kufungua shughuli nyingine za kiuchumi miongoni mwa jamii zetu,"a,esema Mwalimu Makuru.

Aliongeza kuwa,wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne mikoa ya Kusini ilianza kufunguka na kukua kiuchumi ambapo wawekezaji wengi na makampuni mengi ya kigeni na ya ndani yalijitokeza kuwekeza katika viwanda hususani mkoa wa Lindi.

"Huko, kiwanda cha kuchakata gesi kilitakiwa kujengwa kipindi hicho ambacho kingeweza kuzalisha gesi pamoja na mbolea, lakini ghafla baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuondoka madarakani mambo hayakwenda vizuri, lakini tumeona dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kufanikisha jitihada mbalimbali ambazo zitaleta matokeo ya haraka,"alisema.

Pia alisema, katika mkoa wa Ruvuma, Serikali imeamua kufungua uchumi wa mkoa huo hususani katika miradi ya makaa ya mawe na chuma huko Mchuchuma na Liganga ambapo Rais Samia amesisitiza kugawanyika kwa uwekezaji mkubwa katika nyanja za chuma na makaa ya mawe.

Alisema, Rais Samia alisema chuma kina soko kubwa katika soko la Dunia na kina mahitaji makubwa Duniani na hivyo tayari wawekezaji wamekwishaonesha nia ya kuwekeza ndani ya mkoa huo wa Ruvuma, hivyo hatua hiyo itafungua shughuli za kiuchumi,ajira na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi.

Mwalimu Makuru alibainisha kwamba, Serikali imemaliza upanuzi na ujenzi wa bandari ya Mtwara kwa asilimia mia ambapo itasaidia shughuli za usafirishaji wa bidhaa na malighafi hususani korosho kupitia bandari hiyo ya Mtwara, kwani itapunguza bei ya usafirishaji wa mizigo kwa wananchi wa kawaida na wafanyabiashara.

"Pia itasaidia kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na nchi za jirani kama vile Comoro, Madagasca, Msumbiji Malawi na Zambia, bandari ya Mtwara itafungua uchumi wa Kusini na kuongezea nchi kipato na fedha za kigeni.

"Vivyo, hivyo, kutokana na kukamilika bandari ya Mtwara kutasaidia kutunza barabara zetu, kwani mizigo mingi itapitia kwenye bandari hiyo na kuzifanya barabara zetu zidumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo sasa barabara ya Dar es Salaam kuelekea Mtwara ambayo imeharibika sana kutokana na mizigo mingi kupitia barabara itarejea katika viwango bora.

"Kwani kukamilika kwa Bandari ya Mtwara itarahisisha usafirishaji wa mizigo mingi kupitia majini na kuziacha barabara kuwa salama,"alifafanua Mwalimu Makuru.

Wakati huo huo, Mwalimu Makuru amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kuendelea na mipango kabambe ya kutafuta fedha kutoka katika vyanzo vya ndani na wahisani kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa reli kutoka Mtwara kwenda Mbamba bay huko Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.

"Dhamira hii njema, ina lengo la kuunganisha Tanzania na nchi jirani hususani Malawi na Zambia ambapo nchi hizo zitatumia bandari ya Mtwara na treni kutoka Mtwara mpaka bandari ya Mbambabay Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma hivyo itaongeza ajira na mzunguko wa pesa kwa wananchi wa mikoa ya Kusini,"alisema.

Mbali na hayo, Mwalimu Makuru aliishauri Serikali kufufua reli ya Mtwara kwenda Nachingwea mkoani Lindi ambayo ilijengwa na Wakoloni miaka ya 1947 baada ya kumalizika kwa vita ya pili ya Dunia, ambapo wanajeshi wa Uingereza waliotoka vitani walikwenda Nachingwea mkoani Lindi na kuanzisha kilimo cha karanga, hivyo reli ilitumika kusafirisha malighafi hususani karanga toka Nachingwea kwenda Bandari ya Mtwara na kuzipeleka nchini kwako kupitia bandari hiyo.

"Pia kuna haja ya Wizara ya Kilimo kuja na njia mbadala ya kufufua na kuinua zao la karanga kuwa zao la kibiashara ili kuwasaidia wakulima wa mikoa ya Kusini kujiajiri katika kilimo na kuinua hali zao za kiuchumi,"alisema Mwalimu Makuru.

Wakati huo huo, Mwalimu Makuru aliwashauri viongozi wa mikoa ya Kusini kupitia vikao vyao vya mikoa hususani vikao vya RCC waweze kuanzisha shughuli za kiutalii ndani ya mikoa yao kwani wana vyanzo vingi vya utalii vya kuvutia hususani fukwe nzuri za bahari ambazo zinaweza kuvutia uwekezaji wa utalii ndani ya mikoa yao.

Pia Mwalimu Makuru aliiomba na kuishauri Serikali kurudisha mabaki ya Mjusi mkubwa duniani yaliyochukuliwa na Wajerumani kutoka mkoani Lindi maeneo ya Tendeguro mnamo mwaka 1929 na kupelekwa mjini Berlin huko Ujerumani.

Alisema, mjusi huyo ana urefu wa mita 22 kutoka mkiani hadi kichwani na mita 14 kwenda juu, hivyo amekuwa akiliingizia fedha nyingi taifa la Ujerumani pasipo watanzania kunufaika na mali kale na mali asili hiyo ya Tanzania.

Mwalimu Makuru ameiomba Serikali kurudisha mabaki hayo ya mjusi mkoani Lindi kuweza kuongeza vivutio vya utalii ndani ya mikoa ya Kusini kama lilivyoweza Serikali kurudisha fuvu la Chifu Mkwawa mkoani Iringa.

Aidha, Kada huyo aliwashauri viongozi wa Serikali wanapotaka kuanzisha mradi kwa wananchi wawe wanawashirikisha wananchi wenyewe ili kupunguza migogoro.

"Kwa mfano kuna mgogoro wa soko la Chuno baina ya wafanyabiashara na Serikali. Kwani kungekuwa na ushirikishwaji wa wananchi na serikali pasingekuwa na migogoro kati ya serikali na wananchi, hivyo ushirikishwaji ni jambo jema na lenye heri kwa mafanikio ya wananchi na Taifa kwa ujumla,"alisema Mwalimu Makuru.

Mwalimu Makuru ameishukuru Serikali kwa kuwajengea wananchi wa mikoa ya Kusini Hospitali ya Kanda ya Kusini ambapo amesema itarahisisha huduma za afya kwa wananchi wa mikoa hiyo ya Kusini, kwani kabla ya hapo walikuwa wakisafiri kwa umbali mrefu kutafuta huduma za afya za kibingwa, hivyo hospitali hiyo imewapunguzia gharama za kusafiri mikoa mingine na nchi jirani kuweza kutafuta huduma hizo kwani kwa sasa zitapatikana kwenye kanda yao ya Kusini.

Alisema, juhudi hizo za Serikali kuendelea kuharakisha maendeleo ya wananchi kuanzia Kusini, Kaskazini, Mashariki, Magharibi, Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini inatoa faraja na hamasa ya kila mwananchi kuona kuna haja ya kushiriki kwa ufanisi katika kushirikiana na Serikali kuharakisha maendeleo.

"Mfano kuna ujenzi wa barabara mbalimbali unaoendelea mikoa ya Kusini kama barabara kutoka Mtwara, Tandahimba, Newala mpaka Masasi. Kwa asilimia kubwa zimekamilika, hii ni ishara tosha kuwa licha ya kurahisisha shughuli za uchukuzi kutoka mashambani hususani zao la korosho itasaidia kuharakisha maendeleo.

"Nitumie nafasi hii kuiomba Serikali ione umuhimu wa kuitengeneza stendi ya mabasi Mkoa wa Mtwara ili kupunguza hadha kwa wasafiri, maana stendi hiyo inaingiza pesa nyingi kwa Serikali, hivyo kuna ulazima wa kuiboresha.

"Vivyo hivyo, naiomba Serikali kukiboresha Chuo cha Utafiti wa Mimea na Kilimo cha Naliendele kiweze kuboreshwa kwa ajili ya kuongeza udahili kwa wanafunzi na kusaidia wakulima wa mikoa ya Kusini katika kilimo ili kuongeza tija, hivyo kina umuhimu sana tena ikifaa kipewe hadhi hadi kuwa Chuo Kikuu,"alifafanua Mwalimu Makuru.

Post a Comment

0 Comments