NDEJEMBI AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUSHIRIKIANA KIUTENDAJI ILI KUEPUKA MIGOGORO

Na James K. Mwanamyoto,Mpanda

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amezitaka Taasisi zote zote za Umma nchini kuwa na utamaduni wa kushirikiana na kupeana mrejesho wa utendaji kazi, ili kuepuka migogoro ya kiutendaji baina yao kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya utendaji kazi wa Taasisi za Serikali kwa Umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Katavi wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa Taasisi za Umma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Umma mkoani Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amesema, ni jambo la kushangaza pale kiongozi anapokwenda kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Serikali katika eneo lake la utawala na kubaini baadhi ya taasisi kutoshirikiana kiutendaji na badala yake zinatupiana lawama.

“Inakuwaje Watumishi wanaohusika na masuala ya ardhi wanakwenda kubomoa nyumba inayodaiwa kujengwa kinyume na utaratibu, wakati nyumba hiyo imepewa huduma ya maji na umeme na Taasisi nyingine za Serikali”, Mhe. Ndejembi amefafanua.
Baadhi ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Ameongeza kuwa, mgogoro kama huo unatokana na baadhi ya Taasisi za Umma kutoshirikiana na kutopeana mrejesho kiutendaji.

Pia, Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Taasisi za Umma zinategemeana kiutendaji hivyo zinapaswa kujenga utamaduni wa kupeana mrejesho ili kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau.

Pamoja na kusisitiza taasisi za umma kushirikiana, Mhe. Ndejembi amehimiza ushirikiano wa kiutendaji ndani ya Taasisi za Umma na kuhoji kwanini kuwe na kazi inafanywa na taasisi mojawapo ya Serikali ndani ya Sekretarieti ya Mkoa lakini Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) hajapewa taarifa, hivyo amezitaka taasisi za umma kuacha kufanya kazi kimazoea.
Mmoja wa Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Bi. Mercy Salimu akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Naibu Waziri huyo na watumishi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za Watumishi wa Umma mkoani Katavi wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Catherine Mashalla akitoa shukrani kwa Mhe. Ndejembi kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi mara baada ya Naibu waziri huyo kuzungumza na Watumishi wa Umma mkoani humo.

“Ni mara nyingi mambo yanaendelea ndani ya taasisi hususani yenye maslahi wakati viongozi wa juu wa taasisi hiyo hawana taarifa yoyote, lakini jambo likiharibika wao ndio wanawajibika kutoa taarifa Serikalini”, Mhe. Ndejembi amefafanua.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji na kutoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa ni dira ya utendaji kazi unazingatia weledi kwa watumishi wote mkoani humo.

Bi. Mashalla amemuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, yeye na viongozi wenzie watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ili wananchi wapate huduma bora.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Mkoani Katavi yenye lengo la kukutana na Watumishi wa Umma ili kusikiliza kero, changamoto zinazowakabili na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news