Rais mteule Zambia aanza na uhuru wa vyombo vya habari, aifungulia PRIME TV

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais mteule wa Zambia, Hakainde Hichilema ametangaza kurejea rasmi kwa matangazo ya runinga binafsi ya Prime TV baada ya kufungiwa leseni na Serikali inayoondoka madarakani chini ya Rais Edgar Lungu kwa kukataa kutangaza bure matangazo yanayohusiana na ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).
Uamuzi huo wa Rais mteule ambaye ametajwa kuwa mtetezi mpya wa haki za binadamu na makundi mbalimbali ambayo yalikuwa yanataabika miaka kadhaa iliyopita umekuja baada ya kushinda nafasi hiyo siku chache zilizopita.

Prime TV ni kituo cha runinga kisicho cha Serikali kilichokuwa kinarusha matangazo yake kutokea mjini Lusaka, Zambia, ambacho kilianzishwa na kuanza kurusha matangazo yake tangu Januari 20, 2013.

Utawala wa Rais Lungu ulikituhumu kituo cha Prime TV kuwa,kilikuwa kikirusha matangazo ambayo yalikuwa na viashria vya majaribio ya kuiangusha Serikali, hivyo kufungiwa kurusha matangazo yake Aprili 9, 2020 na Serikali.

Baada ya maagizo ya Serikali, Mamlaka ya Huru ya Utangazaji Zambia (IBA) ilisitisha leseni ya utangazaji ya runinga hiyo mara moja.

Katika barua kwa mmiliki wa runinga ya Prime TV, Gerald Shawa kutoka kwa Mjumbe wa Bodi ya IBA, Josephine Mapoma alisema kuwa "kufutwa kwa leseni ni muhimu kwa maslahi ya usalama wa umma. Usalama wa Taifa, amani, ustawi mzuri wa Taifa ”.
Serikali ilikuwa imesimamisha matangazo yote kwa kituo hicho na kuamuru maafisa wake kutojishughulisha na kazi yoyote, hivyo kusababisha mamia ya wafanyakazi na wategemezi kupoteza ajira.

Akizungumzia juu ya hatua hiyo, Shawa alisema kuwa, msimamo wa Prime TV unaonyesha uamuzi wa pamoja wa vyombo vya habari vya kibinafsi, akibainisha kuwa madai yaliyotolewa hayakuwa na ukweli, kwani Serikali iliwanyima fursa pia katika kipindi cha uchaguzi uliopita, badala yake wachache walipendelewa huku wao wakifanya kazi katika mazingira magumu. Hivyo hawakuona umuhimu wa kurusha matangazo ya kampeni dhidi ya virusi vya Corona bure.

Uamuzi huo wa kuifungia runinga hiyo ulilaaniwa na mashirika mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari (IPI), mtandao wa wahariri wa kimataifa, watendaji wa vyombo vya habari na waandishi wa habari wanaoongoza kwa kusimamia uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa nyakati tofauti wananchi mjini Lusaka wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, uamuzi wa Rais mteule kukifungulia chombo hicho cha habari ni ishara njema kwa mwelekeo mpya wa kuijenga Zambia mpya ambayo itadumisha uhuru wa vyombo vya habari, ustawi wa haki za binadamu, demokrasia na uchumi jumuishi kwa wananchi wote.

Esau Chulu ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Zambia, Jumatatu tarehe 16 Agosti 2021 amemtangaza Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia kwa kupata kura 2,810,777.

Alimshinda Bwana Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF) aliyejinyakulia kura 1,814,201.

Kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia, kiliwashirikisha wagombea 16 katika uchaguzi mkuu uliofanyika, Jumapili tarehe 8 Agosti 2021. Wananchi milioni saba nchini Zambia walikuwa wamejiandikisha kupiga kura kati ya wakaazi milioni 19.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news