Rhobi Samwelly azindua Ligi ya Malkia Cup atoa neno kwa vijana

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa Kijisia mkoani Mara, Rhobi Samwelly amewaasa vijana kutojihusisha na vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani katika Jamii, na badala yake washiriki kikamilifu katika shughuli halali za maendeleo ikiwemo uzalishaji mali pamoja na michezo.
Rhobi Samwelly akicheza mpira kichwani wakati wa uzinduzi wa Ligi ya Malkia Cup inayojumuisha vitongoji vitano vya Kijiji cha Kinyariri.
Rhobi Samwelly akikabidhi jezi kwa viongozi wa timu zinazoshiriki Ligi ya Malkia Cup inayojumuisha timu za vitongoji vitano vya Kijiji cha Kinyariri Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama.

Pia, amewaomba kuwa sehemu ya kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo mbalimbali vya kikatili ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu. huku pia akiwahimiza kuzingatia maadili mema na tabia njema ambazo zinakubalika katika jamii na kwa wanamichezo.

Rhobi ambaye aliwahi kutunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu kutokana na juhudi zake za kupambana na ukatili wa kijinsia, ameyasema hayo leo AgOsti 31, 2021 wakati akizungumza katika uzinduzi wa Ligi ya 'Malkia Cup aliyoiandaa yeye ikifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kinyariri na ikijumuisha vitongoji vitano vya Kijiji cha Kinyariri katika kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama. 

Ambapo ligi hiyo ina lengo la kuwajenga vijana kiafya, kiakili, kushiriki mapambano dhidi ya ukatili na kutojihusisha na vitendo vya kihalifu katika Jamii ambavyo havikubaliki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi ya Malkia Cup. Ligi hiyo inajumuisha vitongoji vitano vya Kijiji Cha Kinyariri.
Rhobi Samwelly akiwa amebeba mpira mkononi wakati wa uzinduzi wa Ligi ya Malkia Cup.
Rhobi Samwelly akikagua timu zinazoshiriki Ligi ya Malkia Cup ambapo inajumuisha timu za vitongoji vitano vya Kijiji Cha Kinyariri.

"Vijana niwaombe mdumishe amani katika maeneo yenu mjiepushe na uhalifu, na pia mshiriki kupinga vitendo vya kikatili ambavyo huwafanya wasichana washindwe kufikia malengo yao ikiwemo ndoa za utotoni na ukeketaji mtoe elimu ya madhara kwa jamii. 
 
"Pia mtambue mchango wa wanawake kuanzia ngazi ya familia na kazi mbalimbali za uzalishaji mali wanazofanya. Muishi vyema na dada zenu, mama na pia muwe walinzi wa watoto wasifanyiwe ukatili. Kupitia ligi hii, mshiriki kwa ufanisi kujenga afya kwani sote tunajua mazoezi ni muhimi na michezo ni ajira,"amesema Rhobi.

Aidha, Rhobi ameiasa jamii kuwa na msukumo thabiti katika kuwasomesha watoto wa kike na kutambua mchango wao katika Maendeleo ya Jamii na taifa. Ambapo amesisitiza kila mwananchi kushiriki katika utatuzi wa changamoto zinazo wakabili ili wafikie malengo yao akitolea mfano wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kiongozi bora anayeiongoza nchi kutokana na kusomeshwa na hivi sasa anaiongoza nchi kwa ufanisi mkubwa kwa masilahi ya Watanzania.
Rhobi Samwelly akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ligi ya Malkia Cup inayojumuisha timu za vitongoji vitano vya Kijiji cha Kinyariri kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyariri, Winfrida Wangwe
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyariri, Winfrida Wangwe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ligi ya Malkia Cup inayojumuisha timu tano za vitongoji vya Kijiji cha Kinyariri. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly.
Mwamuzi wa Ligi ya Malkia Cup akikabidhiwa vitendea kazi ikiwemo kadi na vipenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyariri, Winfrida Wangwe amesema kuwa, ligi hiyo itasaidia kuibua vipaji vya michezo kutoka kwa vijana wanaoshiriki ligi hiyo. Ambapo pia amewashauri kupenda kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujiweka timamu kimwili na kiakili wakati wote sambamba na kuzingatia nidhamu wakati wote wa michezo ya ligi hiyo.

Mathias Paul na Mwikwabi Mgendi ambao wanashiriki katika michezo ya ligi hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti na DIRAMAKINI BLOG wamemshukuru Mkurugenzi wa shirika hilo kwa kuanzisha ligi hiyo inayojumuisha vitongoji vyote vya Kinyariri ambapo wamesema itawaimarisha kiafya na kudumisha mahusiano yenye tija miongoni mwao.

Ligi hiyo imeanza kwa kuzikutanisha timu za kitongoji cha Kinyariri chini na Kusaya ambapo timu zinazoshiriki ligi hiyo ni kitongoji cha Bukambiro, Malezi, Kurusanzati, Kinyariri chini na Kusaya, ambapo fainali ya ligi hiyo inatarajia kufikia tamati Septemba 17, mwaka huu na bingwa atakabidhiwa kitita cha shingi 200,000 na kikombe, mshindi wa pili 100,000 na mshindi wa tatu 50,000.

Post a Comment

0 Comments