Serikali yadhamiria kudhibiti udumavu kwa watoto nchini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

IMEELEZWA kuwa Serikali imeendelea kupambana na changamoto mbalimbali za kiafya kwa mtoto ili kuhakikisha anakuwa katika afya njema kuanzia utotoni hadi utu uzima.

Lengo ni kuhakikisha takwimu za mwaka 2018 ambazo zinaeleza kuwa Kitaifa asilimia 31.8 ya watoto wana udumavu zinashuka hadi kufikia sufuri.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mratibu wa Lishe ya Mama, Mtoto na Kijana Balehe kutoka Wizara ya Afya,Tufingene Malambugi wakati akitoa semina kwa waandishi wa habari jijini Dodoma ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama Duniani ambayo ilizinduliwa Agosti 1, mwaka huu mkoani Songwe.
Amesema kuwa, licha ya changamoto hiyo,Tanzania imepiga hatua katika unyonyeshaji ambapo asilimia 97 ya wanawake unyonyesha watoto wao kwa ufasaha kutokana na utafiti uliofanywa na Hali ya Lishe TNNS 2018.

Akizungumzia athari za kutonyonyesha mtoto kwa ufasaha amesema, huwa inapelekea udumavu wa mtoto, kupelekea ukuaji wa makuzi kuwa duni,kuongezeka kwa magonjwa na udhaifu na akiwa mtu mzima kuugua magonjwa ya kisukari na kupunguza uwezo wake wa kufikiri na hatimaye kushindwa kuzalisha mali na kipato chake kuwa duni na kwa wanawake kuzaliana kizazi hadi kizazi.

Akitoa taarifa ya hali ya ulishaji wa watoto wachanga katika miezi sita ya mwanzo,Afisa Tafiti Mwandamizi Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Ruth Mkopi amesema kuwa, takwimu za kidunia toka mwaka 2018 zinaonesha kuwa asilimia 44 ya watoto chini ya miezi 6 wananyonya maziwa ya mama huku Tanzania ikiwa ni asilimia 58.

Amesema, faida ya maziwa ya mama kwa mtoto ni pamoja na kuweka kinga ya mwili,kuleta uhusiano mzuri kati ya mama na mtoto, kusaidia kuchelewesha kupata mimba nyingine kwa mama,kuepusha kupata ugonjwa wa saratani na kusaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali yake ya kawaida.

Nae Afisa Mtafiti Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Walbert Mgeni amesema, katika familia na jamii kuna vikwazo mbalimbali vinavyofanya mazingira ya unyonyeshaji yasiwe rafiki ikiwa ni kazi nyingi zinazowakabili wanawake,mila na imani potofu juu ya unyonyeshaji wa watoto wadogo,ukosefu wa utashi kwa baadhi ya wanajamii.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuondokana na upotoshaji uliopo kwenye jamii juu ya maziwa ya makopo kwamba yana kinga jambo ambalo sio sahihi na badala yake watambue kuwa maziwa ya mama pekee ndiyo yanaweza kumlinda mtoto dhidi ya maradhi.

Awali akielezea lengo la semina hiyo kwa waaandishi wa habari,Kaimu Mkurugenzi Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya, Grace Moshi alisema kuwa,itawasaidia kufikisha elimu kwa jamii kupitia kalamu zao.
Pia amesema, itasaidia kutangaza,kutoa elimu kwa jamii kuendeleza taratibu sahihi za unyonyeshaji watoto maziwa ya mama na kujenga mazingira wezeshi kwa wanawake ili waweze kuwanyonyoesha watoto wao kwa ufanisi.

Hata hivyo, amesema malengo ya wiki ilikuwa kulinda na kuendelea na kuhamasisha unyonyeshaji kwa mama, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda unyonyeshaji wa maziwa ya mama, kuhamasisha jamii ichukue hatua za kulinda unyonyeshaji ili kuboresha afya ya umma, kuhimiza ushirikiano wa wadau ikiwemo sekta binafsi.

Mbali na hayo katika maadhimisho hayo yalienda sambamba na kauli mbiu ya "kulinda unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni jukumu letu sote".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news