Tamaa za baadhi ya wafanyabiashara zamkwaza Rais Dkt.Mwinyi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kusimamia upandishwaji wa bidhaa usio wa halali unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara hapa nchini.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya sala ya Ijumaa huko katika Masjid Noor Abswar maarufu Msikiti wa Abdalla Rashid, Kiembe Samaiki, Wilaya Magharibi “B”, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) alipokuwa akiwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi baada ya kushiriki sala ya Ijumaa katika Masjid Noor--Abswar Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi "B" Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni kawaida yake kushiriki katika Masjid mbalimbali.[Picha na Ikulu].

Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kwa sasa kumetokea baadhi ya wafanyabaiashara ambao wamepadisha bidhaa zao bila ya kufuata taratibu za Serikali na kuuza bidhaa hizo kwa bei za juu ikiwemo bidhaa ya saruji na nyinginezo.

Alisema kuwa, wafanyabiashara hao wamekuwa wakitoa kisingizio cha uwepo wa maradhi ya COVID-19, ambao kumepelekea kupaishwa bei ya bidhaa huko nje ya nchi pamoja na suala zima la usafiri, lakini alisema licha ya kuwepo hali hiyo bado bidhaa zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu hata zile zinazotoka ndani ya nchi, ikiwemo saruji inayotoka Dar es Salaam na Mtwara.

“Hii ni haramu, lakini kibaya zaidi kuna baadhi ya bidhaa wala hazitoki China na Ulaya lakini bidhaa inakuwa juu.... leo kuna saruji inayatoka Dar es Salaam, Mtarwa kuna sababu gani kufika elfu 20 kwa hivyo, nawataka wafanyabiashara wasipandishe biashara ovyo wanawaumiza watu lakini niwatake wasimamizi wa bei katika Wizara zetu za Serikali, Wizara ya Biashara ina jukumu hili la kuhakikisha watu hawapandishi bei ovyo wasikae tu wanaona mambo yanaharibika hawasemi lolote,"alisisitiza Alhaj Dkt. Mwinyi.

Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kusimamia hali hiyo ikiwa ni pamoja na kwenda kuangalia katika maghala ya bidhaa na hata kufungia biashara za watu wanaopandisha bei ovyo bila ya sababu huku akisisitiza haja ya kufanya mambo ya halali na kuepuka haramu.

Aliwasihi wafanyabiashara wasichukulie sababu ya kuwepo kwa maradhi ya COVID-19 na kupandisha bei ya bidhaa kwani wanawaumiza watu kwani hali hiyo inakuwa haramu.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza suala zima la uwajibikaji kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi waliokabidhiwa hasa wale waajiriwa wa Serikali.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa wapo waajiriwa ambao hawatimizi majukumu yao licha ya kuwa wanakwenda kazini lakini wamekuwa hawatoi huduma stahiki kwa wananchi kama inavyotakiwa sambamba na kuiepelekea nchi kukosa mafanikio.

Kutokana na hali hiyo, Alhaj Dkt. Mwinyi alisisitiza matakwa ya dini yanataka kila kinachopatikana kiwe cha halali na kueleza kwamba maendeleo katika nchi yatakuwa ya haraka iwapo kila mmoja atawajibika ipasavyo.

Mapema, akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alieleza haja kwa kila mmoja kujitahidi kula vitu vya halali na kujiepusha na kula vitu vya haramu na kueleza athari anazozipata mwanaadamu kabla na baada ya kufa kwake.

Alisema kuwa mwanadamu atakwenda kuulizwa mbele ya mola wake ni vipi amepata mali alizokuwa nazo duniani, huku akisisitiza kwamba hatoingia peponi mja ambaye mwili wake ulipata siha kutokana na chumo la haramu.

“Kila ammoja ajilazimishe kutafuta halali japo kuwa iwe ndogo...kila mmoja ajitahidi kufanya kazi ili apate rizki ya halali...kwa wale wote waliopewa kusimamia mali ya umma ni haramu kuidokoa....ni vyema watu wakafanya akzi wkani hata Mitume wote wa Allah walifanya kazi,”alisisitiza Sheikh Khalid Ali Mfaume.

Nae kiongozi wa Kamati ya Msikiti huo, Mzee Abdalla Rashid alimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuungana nao pamoja msikitini hapo kwa ajili ya kusali Sala ya Ijumaa na kumueleza jinsi wananchi wa msikiti huo walivyofarajika wka ujio wa kiongozi huyo.

Post a Comment

0 Comments