TANZIA: Mkurugenzi wa Jambo Express, James Mtei afariki

Na Mary Margwe, Babati

Mfanyabiashara maarufu mkoani Manyara, James Mtei ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Jambo Express amefariki dunia ghafla.
Awali, Mtei alikuwa mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya mabasi ya Mtei akiwa nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Elly Mtei alisema kaka yake, James Mtei amefariki leo Agosti 25, 2021, ambapo alisema kaka yake amefariki ghafla kwa ugonjwa wa shinikizo la damu akiwa nyumbani kwake Mrara Mjini Babati.

Aidha, alisema familia imempoteza ndugu yao ambaye alikuwa ndio kiungo katika kuwaunganisha wao kama wadogo zake, hivyo kuondoka kwa kaka yao imekua ni pigo kubwa sana katika familia ya Mtei.

"Hakika hatuna namna kabisa, zaidi ya kumuachia Mungu kwenye kujua siri ya maisha yetu binadamu, maana amefariki ghafla kwa ugonjwa wa shinikizo la damu akiwa nyumbani kwake Mrara, sijui nini niseme jamani," alisema Elly Mtei mdogo wa marehemu James Mtei.

Aidha, alisema kwa sasa ndugu wanaendelea kukutana nyumbani kwa marehemu Mrara Mjini Babati ulipo msiba, ili kupanga taratibu za mazishi, ndipo baadaye wengine watajulishwa, hivyo wao kama familia wanaendelea na vikao vya ndugu, jamaa na marafiki.

"Baadhi ya ndugu wapo hapa mjini Babati kwa mipango ya taratibu za mazishi ili kupanga taratibu za siku na mahali maziko yatakapofanyika," amesema Mtei.

Kwa upande wake mbunge mstaafu wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jituson amesema mji wa Babati na mkoa mzima wa Manyara, umepoteza mdau muhimu na maarufu wa maendeleo mkoani humo.

Jituson amesema wanamuombea marehemu Mtei apumzike kwa amani na huku akitoa rai kwa jamii kuiga yale mazuri yote aliyofanya kipindi cha uhai wake marehemu James.

"Alikuwa ana utu mwenye kujitoa kwa hali na mali ikiwemo usafiri na huduma za jamii, michango ya ujenzi wa shule, zahanati na maendeleo mengine, Manyara tumepata pigo kubwa," amesema Jituson.

Naye jamaa wa karibu na marehemu huyo Peter Ringi alisema amemfahamu marehemu miaka mingi, ambapo amemuelezea mengi mazuri hususani ushiriki wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika wilaya na mkoa kiujumla.

Hata hivyo, Ringi alisema ni vema watu kama hao wanapoondoka jamii inayobakia ikaiga yale mema yote, kwani marehemu alikua ni mtu wa watu katika kuhakikisha maendeleo ya mkoa huo yanakwenda, familia hiyo ina kchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa huo.

Post a Comment

0 Comments