TANZIA: Mwalimu Alex Kashasha afariki


Mchambuzi nguli wa soka Tanzania, Mwalimu Alex Kashasha amefariki dunia leo Agosti 19, 2021.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii kimeidokeza DIRAMAKINI Blog kuwa, amefariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam.  

Mwalimu Kashasha alijizolea umaarufu kutokana na umahiri wake wa kuchambua mpira wa miguu kwa michezo ya ndani na nje ya nchi.

Kashasha alikuwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) hadi umauti ulipomfika.


KUHUSU MWALIMU KASHASHA TAZAMA 

Kashasha aliwahi kuwa mchezaji soka, mchambuzi wa soka, mwalimu wa michezo na mkufunzi wa vyuo vya ualimu.

“Ni kweli bao hili limefungwa kiufundi zaidi, haswa kwa kutumia mtindo 4,4,2..” ndivyo alivyokuwa akiongea kwa kutumia ujuzi wake wa ualimu wa michezo aliosomea miaka ya themanini na kuchambua mchezo wa soka ambapo hapo awali lilikuwa jambo geni nchini Tanzania.

Mwandishi ADELADIUS MAKWEGA anasema kumfahamu Mwalimu Kashasha alifunga safari ya kifikra mpaka mwaka 2014 ambapo aliweza kumuona kwa mara ya kwanza wakati wa Kombe la Dunia.

Makwega alikuwa mtangazaji na mtayarishaji vipindi wa TBC Taifa.

Anasema, anachoweza kukumbuka ni kuwa mtangazaji aliyekuwa naye karibu sana alikuwa ni Jesse John kwani ndiye alikuwa mtayarishaji na mtangazaji wa soka tangu Kombe la Dunia la mwaka 2010, enzi zile za TBC chini ya Mkurugenzi Tido Mhando.

“Ni kweli mimi ndiye niliyeweza kuhakikisha mwalimu Kashasha anakuja TBC Taifa na kila wakati kulipokuwa na mechi ya kabumbu aliweza kupata nafasi ya kuwepo uwanjani kwa mechi za nyumbani na hata studioni kwa mechi za kimataifa kuchambua mechi husika,” anasema Jesse John.

Kabla ya kuja TBC, katika harakati mbalimbali za maisha Jesse John anasema alikutana na Mwalimu Kashasha mwaka 1988 akiwa mkufunzi wa mafunzo ya Ualimu wa Daraja A Chuo cha Ualimu Butimba.

Wakati huo huo Mwalimu Kashasha alifika kujiendeleza katika Ualimu wa Michezo akitokea kazini maana yake alikuja katika mafunzo kazini.

Kwa wakati huo Waziri Mkuu wa sasa Kassim Majaliwa alikuwa miongoni mwa wakufunzi waliokuja kujifunza ualimu huo wa michezo anasema Jesse John.

“Tukiwa Chuoni Mwalimu Kashasha alikuwa akicheza mpira huku akiwa kocha wetu, mimi (Jesse John) nikiwa golikipa wa timu ya Chuo cha Ualimu Butimba, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mchezaji nambari saba," anaongeza Jesse John.

Maisha yana safari ndefu sana, nilikutana na mwalimu Kashasha tena Kombe la Dunia la mwaka 2014 akiwa mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Vikindu Mkoa Pwani na kwa kuwa nilikuwa namfahamu kama mwalimu wa michezo na mtu anayeifahamu michezo kitaalamu sikuwa na ajizi ndipo akaja TBC tukaanza kuchambua michezo katika redio yaani TBC Taifa.

“Wadau wengi wa mpira wamejifunza soka kupitia kwake, kwani wakati anachambua mpira wengine walikuwa wakiandika kutokana na uchambuzi wake na alikuwa hachambui kwa kusoma katika mitandao bali aliusoma na kuucheza huo mpira wa miguu,"alisisitiza Jesse John.

Mwalimu Kashasha aliucheza mpira wa miguu akiwa shuleni, chuo cha Ualimu Butimba na aliweza kufundisha mpira wa miguu katika timu mbalimbali kwa mfano Majimaji ya Songea kwa kipindi kifupi, timu ya Maji Mara, timu ya Mkoa wa Mara wakati wa mashindano ya Taifa CUP. Kwa hakika kifo chake ni msiba mkubwa kwangu mie na wadau wengine wa soka.

“Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni saa 9 alasiri Agosti 18, 2021 alikuwa akiniuliza juu ya usajiri wa timu za Simba na Yanga, huku akiniandikia yale tuliyokuwa tunazungumza katika karatasi. Alikuwa akizungumza kwa tabu sana,"alieleza Jesse John.

“Wapenzi wa mpira miguu wanajua kuwa mpira huu ulikuwa na vionjo kupitia kwa uchambuzi wa Mwalimu Kashasha, watu waliokuwa wakitazama runinga, lakini cha kushangaza walikuwa wakitumia sauti ya matangazo ya TBC Taifa kupata utamu na vionjo vya uchambuzi wa mwalimu Kashasha,"aliongeza Mtangazaji Jesse John.

Mwalimu Alex Kashasha ameacha Mjane na watoto mabinti wawili. Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga milele umwangazie, apumzike kwa amani, Amen.

Post a Comment

0 Comments