UVCCM yaitaka CHADEMA kuwafunda BAVICHA

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM),Keenan Kihongosi amewataka viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwafunza vijana wa Baraza la Vijana wa chama hicho (BAVICHA) wawe na adabu ya kuheshimu sheria za nchi na kuacha kuvuruga amani.

Hatua hii imekuja kufuatia tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Pambalu kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kukidhi matakwa yao huku likiwataka vijana wa chama hicho kuandamana Agosti 5, mwaka huu kwa madai ya kudai demokrasia kuhusu kesi inayokabili Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

Akizungumza kwenye mkutano wake na vyombo vya habari jijini hapa,Katibu huyo wa UVCCM-Taifa ameeleza kuwa ni aibu kwa watu wazima kuendelea kung'ang'ania mambo ambayo hayawezekani huku akiwataka kufuata taratibu za mahakama ikiwa wanahisi kuonewa.

Amesema, hakuna mtu aliye juu ya sheria na kuwa na mamlaka ya kumtaka Mheshimiwa Rais kufanya jambo au matakwa yao binafisi.

"Wapinzani wanapaswa wajitafakari,wabadilike na kukubali kubadilisha aina ya mfumo wa siasa wanaoutumia,lazima katika siasa kuna ushindani,wahakikishe wanakuwa Mabalozi wa amani na kuepuka kuhamasisha vurugu,"amesema.

Kutokana na hayo Kihongosi amewataka wanachama hao wanaotaka kuandamana kuendelea kufanya shughuli za maendeleo kwa ajili ya manufaa kwa familia zao badala ya kutumia muda huo kwa masuala yasiyo na msingi.

"Niwashauri tu vijana wenzangu, badala ya kuandamana muda huo tumieni kutafuta ugali wa familia zenu,"amesema.

Katibu huyo ameeleza kuwa, Mwenyekiti wa BAVICHA lazima atambue kwamba nchi hii inaongozwa na Sheria na kwamba siku zote wao wamekuwa wakijipambanua kuwa wanataka Demokrasia Sasa anashangaa wanataka kuvunja Sheria na kusahau kuwa kila mhimili unafanya kazi kwa namna yake.

"Mnapotaka kuandamana kupinga kuhusu yanayomhusu Mbowe mmejiridhisha vipi kwamba hana makosa,mna wajibu wa kutii sheria za nchi,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news