Viongozi wa dini endeleeni kumuombea Rais Samia, wasaidizi wake, nchi yetu-Mwenyekiti CCM Mara

*Aongoza harambee ujenzi wa Kanisa la Kemange SDA,ampongeza Rais Samia kwa kuwaletea RC Hapi,awataka waumini kuacha roho ya uchoyo, wamtolee Mungu zaka na sadaka, wachape kazi


NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) ameendelea kuwaomba viongozi wa dini wakiwemo wachungaji, maaskofu, masheikh na wengine wote kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwani maombi yao ni muhimu sana katika kumpa nguvu na maarifa ya kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
"Nichukue fursa hii kuendelea kuwaomba wachungaji,maaskofu, masheikh na viongozi wote wa dini kuzidi kuiombea nchi yetu ya Tanzania iendelee kuwa na amani pamoja na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuchapa kazi na kuwaletea Watanzania maendeleo pamoja na wasaidizi wake;

Mheshimiwa Kiboye ameyasema hayo wakati akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kemange SDA mkoani Mara ili kusaidia kuharakisha ujenzi wa kanisa katika eneo hilo.
"Pia niwaombe waumini tujenge kanisa kwa pamoja na tuwe na moyo wa kumtolea Mungu zaka na sadaka, ndipo tutabarikiwa zaidi,"amesema Mwenyekiti Kiboye.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa, nguvu ya maombi kwa Taifa na viongozi wake ni kubwa katika kuwapa mwanga wa kuliongoza Taifa huku wakiwa na hofu ya Mungu ambayo ni hatua tosha ya kuharakisha maendeleo.
"Kila mmoja wetu anatambua kuwa, Yesu anafungua njia pasipo na njia na anatoa majibu kwa wakati wowote, hii ikimaanisha kuwa, anasikia maombi yetu kila dakika au sekunde, hivyo tuendelee kumuombea Rais wetu na Taifa ili liweze kusonga mbele kiuchumi.

"Ninaamini tukiendelee kuwa na hofu ya Mungu hata haya matendo ya ovyo ovyo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika jamii kama lile la yule kijana aliyewaua askari wetu huko Dar es Salaam hayawezi kujitokeza, kwa Mungu ndiyo mwisho wa mambo yote, hivyo tuendelee kumuomba Mungu na kuhubiri habari njema kwa ajili ya kuwaunganisha watu na kuwaleta Watanzania mbele za Mungu, hiyo ni hatua muhimu sana katika ukuaji wa uchumi na amani ya Taifa letu,"amesema Kiboye.
Wakati huo huo, aliwasisitia waumini wote kuendelea kujitoa kwa Mungu bila kujali hali zao au vyeo vyao kwani, Mungu huwa anatimiza jambo lolote kwa wakati.

"Inabidi tuendelee kuikataa hii roho ya watu wanaosali kuendelea kuwa maskini sana, kwa sababu hayo wanajitakia wenyewe, kwani hawapendi kutoa zaka na sadaka kwa Mungu, someni Isaya 45:3. Mungu hawezi kukubariki kama huwezi kumtolea na watu wamekuwa wachoyo, hawataki kumtolea Mungu ipasavyo badilikeni, someni Hagai 2:8,"alifafanua Kiboye.
Katika hatua nyingine, Kiboye alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mkuu wa mkoa mchapa kazi na mwenye maono makubwa kwa mkoa huo.

"Kwa kweli nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea Ally Hapi kuwa mkuu wa Mkoa wa Mara, tumeanza kuona mabadiliko na ni mchapa kazi pia anajali Chama Cha Mapinduzi,"alisema Kiboye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news