Waziri Mkuu atoa siku nne waliokuwa vigogo Wilaya ya Temeke wafikishwe mahakamani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na gharama za ujenzi wa miradi ya barabara ya Kijichi–Mwanamtoti yenye urefu wa kilomita 1.8 iliyogharimu shilingi bilioni 5.4 na barabara ya Kijichi-Toangoma yenye urefu wa kilomita 3.25 iliyogharimu shilingi bilioni 13.5.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameiagiza Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ihakikishe watu wote waliohusika na ubadhirifu huo wa fedha ambao tayari walishasimamishwa kazi wawe wamefikishwa mahakamani kabla ya Agosti 20, 2021.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Agosti 16, 2021 wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za Kijichi-Mwanamtoti na Kijichi-Toangoma wilayani Temeke na kituo cha Mabasi kilichopo Buza. Mirado hiyo inajengwa kupitia mradi uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

“Manispaa ya Temeke waliamua kutujengea mradi huu kwa kuongeza gharama kubwa za ujenzi. Tumeona namna mlivyoharibu fedha za nchi. Hatuwezi kujenga kilomita 1.8 ya lami kwa gharama ya shilingi bilioni 5.4 na hatuwezi kuwa na watumishi wa umma wa namna hii.

“Watu wote waliohusika warudishwe na wafikishwe mahakamani, hatuwezi kufanya mchezo hizi ni fedha za walipakodi itakuwa ni mchezo kila mmoja anakuja anachukua fedha na kuondoka hatuwezi kujenga barabara ya kilomita 1.8 kwa gharama ya shilingi bilioni 5.4,"amesema.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya ahakikishe anasimamia na anazingatia maslahi ya Wana-Temeke katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Wananchi Serikali yenu iko macho kweli kweli na hakuna sarafu itakayotoweka tunailinda na Mawaziri tupo kwa ajili hiyo na tuna maelekezo thabiti ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na watumishi wa umma tuko hapa kuwahudumia wananchi,”amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza TAKUKURU iwatafute viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke waliohusika katika kukopa shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ulipaji fidia ya ujenzi wa miradi mbalimbali warudishwe ili ajibu tuhuma zinazowakabili.

Mbali na agizo hilo, pia Waziri Mkuu ameelekeza kusimamishwa kwa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi Buza hadi hapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu atakapojiridhisha ni mradi gani unapaswa kufanyika katika eneo hilo.

Pia, Waziri Mkuu ameiataka TAKUKURU ifanye uchunguzi ili kubaini ni kwanini uongozi wa Manispaa hiyo ulianza kulipa mkopo huo miezi miwili baada ya kuupokea mkopo huo huku mkataba ukionesha kuwa wanaweza kulipa deni hilo baada ya miezi sita kulingana na muda wa matazamio.

Akizungumzia kuhusu eneo la Temeke Kota, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na uongozi wa Manispaa ya Temeke wakutane na wafanye uamuzi juu ya matumizi ya eneo hilo na baada ya wiki moja wampelekee taarifa ya walichopanga kukifanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news