Waziri Ndumbaro: Hakuna uthibitisho kuwa pembe za faru zinaongeza nguvu za kiume

Na Lusungu Helela-WMU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameitaka jamii kuachana na imani potofu kuwa pembe za faru zinaongeza nguvu za kiume kwani hakuna uthibitisho wa kisayansi juu ya madai hayo baadala yake ameitaka jamii kuungana na Serikali katika kumlinda faru ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii hapa nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( katika ) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Wadau wa Uhifadhi nchini mara baada ya kushuhudia zoezi la uzinduzi wa uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa ajili ya utambuzi na kufuatilia nyendo za faru kwa ajili ya ulinzi wa faru hao katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Amesema kutokana na imani hiyo potofu imepelekea faru kuwindwa sana na kuna baadhi ya nchi zimekuwa zikinunua pembe hizo za faru kwa bei ya ajabu, hali hii imeilazimu Serikali ya Tanzania kujizatiti katika kuwalinda faru kwa kuwawekea vifaa maalum ajili ya ulinzi ili wasiweze kuuawa

Ametoa kauli hiyo wakati akizindua zoezi la uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa faru katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Wanyama hao ambao ni zao kubwa la Utalii nchini

Dkt.Ndumbaro amesema, kuhifadhi faru kunataka nguvu ya ziada pamoja na akili ya ziada kwa sababu binadamu ni kiumbe mharibifu na tayari ameingiza mawazo yake kuwa nyara zina nguvu ya ziada.

Kufuatia hali hiyo ameaugiza Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ushirikiane na Idara ya Wanyamapori kuhakikisha wanakamilisha kuweka alama na vifaa maalum kwa ajili ya utambuzi na ulinzi kwa faru wapatao 45 badala ya kuwawekea vifaa hivyo faru 20 pekee waliokuwa wamepanga kuanza nao lengo likiwa ni kuhakikisha faru wote katika eneo hilo wanakuwa salama zaidi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ( wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Raymond Mangwala ( wa pili kushoto) wakiwa wamemshika huku wakiwa wanashuhudia zoezi la uzinduzi wa uwekaji wa alama za utambuzi wa faru pamoja na uwekaji wa kifaa maalum cha kufuatilia nyendo za faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Wa tano kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt.Maurus Msuha.

Dkt.Ndumbaro ameeleza kuwa faru wote wanatakiwa kuwekewa vifaa hivyo kwa sababu wale 25 kati ya 45 ambao watakuwa wamesalia wanaweza kukutana na balaa yoyote.

Ambapo ameutaka Uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kama una changamoto yyoyote wamfikishie ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa faru wote kwa sababu mitambo iliyopo ina uwezo wa kufuatilia nyendo za faru zaidi ya 100,000 kwa ajili ya usalama wao.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameuagiza Uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha faru wenye watoto wadogo wanahifadhiwa katika maeneo maalum hadi pale faru wadogo watakapokuwa wakubwa ndipo waweze kurudishwa katika mazingira yao asili ili wasiweze kuliwa na fisi.

Kwa mujibu wa taarifa fisi wamekuwa tishio kubwa kwa watoto wa faru ambapo faru wanapokuwa wadogo wamekuwa wakiliwa na fisi ambapo katika eneo la Ngorongoro kuna idadi kubwa sana ya fisi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( wa nne kulia) akipewa maelezo kutoka kwa Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kabla ya kuanza kwa zoezi la uzinduzi wa uwekaji wa alama pamoja na vifaa maalum kwa ajili ya utambuzi na kufatilia nyendo za faru kwa ajili ya ulinzi wa faru hao katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Amefafanua sababu za kuliwa na faru wadogo ambapo amesema faru wenye watoto wadogo huliwa kwa sababu faru weusi kiasili huacha watoto wadogo nyuma wakati wa kutafuta malisho hivyo fisi hutumia nafasi hiyo kuvamia na kuwala watoto hao.

Amesema kutokana na umuhimu wa fisi kiikilojia na kiutalii haiwezekani kuwaondoa fisi ila jambo linalotakiwa kufanywa ni kuhakikisha faru watoto wanalindwa kwa kuwaondoa katika mazingira hayo hatarishi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameagiza Uongozi wa Hifadhi hiyo kutenga eneo maalum kwa ajili faru wazee ambao kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu kuwa faru wanapozeeka hupoteza uwezo wa kuona hivyo litengwe maalum kwa ajili ya kuwahufadhi faru hao ili litumike kwa ajili ya utalii wa faru.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (tano kutoka kushoto) akiwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Wadau wa Utalii wakishuhudia zoezi la uzinduzi wa uwekaji wa alama za utambuzi wa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Raymond Mangwala


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akimkabidhi cheti Kiongozi wa mradi wa Frankfurt zoological Society Bw. Rian Labuschagne kama ishara ya kutambua mchango wao katika mradi wa uhifadhi wa Faru nchini.

Awali, Kamishna Uhifahi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro , Dkt.Freddy Manongi amesema Ngorongoro ni eneo pekee dunia ambalo watalii wataweza kumuona faru weusi katika mazingira yake asilia

Aidha, Dkt.Manongi amueleza changamoto wanazokabiliana katika kumlinda faru kutoka na ûwepo matumizi mseto katika eneo hali inayochangia katika kuwalinda faru hao.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha ameeleza kuwa zoezi la kuweka alama kwa Faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa na faru hao kuwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news