Bosnia ataka Ukaguzi Maalumu Milioni 400/- jengo la Mama na Mtoto Lushoto

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ametaka ufanyike Ukaguzi Maalumu wa sh. milioni 400 ambazo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwenye Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, lakini ujenzi wake umeshndwa kukamilika.

Moja ya sababu inayodaiwa kugharimu jengo hilo lisimalizike kwa wakati, ni vifaa vyake vya ujenzi kuchukuliwa maeneo ya mbali kwa bei kubwa na kuacha vifaa hivyo karibu kama vile mawe, mchanga, kokoto na bidhaa nyingine.
Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani hivi karibuni, Shekilindi alihoji kuwa ikiwa bado kuna tuhuma kwa fedha hizo sh. milioni 400 kutoka Serikali Kuu kutumika bila kukamilisha kazi iliyokusudiwa, halmashauri hiyo imetoa sh. milioni 54 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo hilo, huku akihofia fedha hizo nazo zitatumika bila kufikia malengo, na kutaka kufanyike Ukaguzi Maalumu.

"Serikali ilitoa fedha sh. milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwenye Hospitali ya Wilaya, lakini ujenzi wa jengo hilo umeshindwa kukamilka. Lakini bado halmashauri imeongeza tena sh. milioni 54 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo. Tunahoji kwa nini sh. milioni 400 hazikumaliza ujenzi wa jengo hilo. Pia ni kwa nini halmashauri imetoa tena sh. milioni 54 wakati ujenzi wa jengo hilo kuna tuhuma mbalimbali kwa kushindwa kukamilika kwake.

"Tunataka Special Auditing (Ukaguzi Maalumu) kwa ajili ya fedha hizo ili kujiridhisha hakuna ubadhirifu umefanyika. Lakini kama itakuwa hivyo, basi hatua zichukuliwe. Hatuwezi kukaa kimya kwa kuona fedha zinaletwa kwa ajili ya kujenga majengo kwa Force Account zinatumika vibaya" alisema Shekilindi maarufu kama Bosnia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro alisema upo ubadhirifu kwenye baadhi ya maeneo ya ukusanyaji ushuru, kwani katika ukaguzi wa kustukiza alioufanya kwenye maeneo ya kukusanyia ushuru kizuizi cha Nyasa, alibaini mkusanya ushuru anatumia kukusanya ushuru huo kwa kutumia Mashine ya POS ambayo ni ya halmashauri. Lakini pia anakusanya kwa tigo pesa ya simu yake binafsi, huku ushuru mwingine akikusanya fedha taslimu.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko alisema baadhi ya fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu ambazo ni asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya halmashauri, na zipo kisheria baada ya kupitishwa na Bunge, haziwafikii walengwa. Hivyo ametaka zichukuliwe hatua za makusudi ili kuweza kufikisha mikopo hiyo kwa walengwa.

Akijibu baadhi ya hoja, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mathew Mbaruku alisema suala la jengo la mama na mtoto linafanyiwa kazi kujua ni nini kimetokea mpaka halijakamilika. Lakini pia sh. milioni 54 zilizotolewa na halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo zipo kwenye mpango wao, kwani wao kama halmashauri, walitakiwa kutoa sh. milioni 194 ili kukamilisha jengo hilo.

Akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge alisema tayari wamewasimamisha baadhi ya vibarua wakusanya ushuru kwenye vizuizi hasa kile cha Nyasa. Nia ikiwa kupisha uchunguzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news